The House of Favourite Newspapers

KIBA ALIVYOKUSANYA ‘KIJIJI’ CHA WATU MAARUFU!

WIKI hii ndiyo tunamaliziamalizia ‘news’ za harusi ya mwanamuziki maarufu Bongo, Ali Saleh Kiba ‘AliKiba’ na mwanadada kutoka Mombasa nchini Kenya, Amina Khaleef ambazo ‘zimetrend’ takriban wiki mbili sasa kwa mambo tofautitofauti.

 

Baada ya ndoa kufungwa nchini Kenya, wiki hii kulikuwa na sherehe ya pili ya kuhitimisha harusi hiyo jijini Dar es Salaam, pale Serena Hotel ambapo Kiba aliwakutanisha watu wengi maarufu kutoka kila kona Afrika Mashariki. Ni kina nani hao? Soma chini;

WANASIASA

Miongoni mwa watu ambao Kiba aliwakutanisha ni wanasiasa. Alikuwepo mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, mama Salma Kikwete ambaye alihudhuria kama mama mlezi wa Kiba.

Mbali na mama Salma, alikuwepo pia mwanaye, Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Chalinze, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla bila kumsahau Gavana wa Mombasa, Hassan Joho.

 

WANAMUZIKI NA WAIGIZAJI

Wanamuziki na waigizaji pia hawakuwa nyuma kuibuka kwenye sherehe hiyo baada ya kupewa mialiko.

Wanamuziki waliokuwepo ni Mwana FA, Christian Bella, Vanessa Mdee, Mimi Mars na Ommy Dimpoz. Huku waigizaji akiwepo Esha Buheti na Idrissa Sultan.

WANASOKA

Kiba alionesha pia kwamba rafiki zake si wanamuziki, waigizaji na wanasiasa tu bali hata wanasoka ni jamaa zake.

Katika kuthibitisha hilo, walikuwepo wadau wa mpira wa miguu nchini na wachezaji. Kwa upande wa wadau alikuwepo Msemaji wa Timu ya Simba, Haji Manara, aliyeingia akitokea uwanjani ambako Simba ilikuwa imewaburuza wapinzani wao Yanga kwa bao 1 kwa sifuri.

Alikuwepo pia nyota wa mpira wa miguu nchini, ambaye ni Mganda, Emmanuel Okwi anayekipiga katika Klabu ya Simba huku Yanga wakiwakilishwa na Haroub Canavaro.

WATANGAZAJI

Watangazaji waliokuwepo kwenye harusi hiyo ni pamoja na Millard Ayo, Husna Dacota na Shadee wote wa Clouds Media, Angela Msangi wa TBC1 na Abdallah Aambua ‘Dulla’ wa kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa kituo cha runinga cha EATV.

Katika halfa hiyo, mama Salma Kikwete ambaye ndiye mama mlezi wa bwana harusi, alipata nafasi ya kutoa nasaha zake kwa maharusi hao ambapo aliwasihi kulinda ndoa yao na linapokuja suala la ndoa waweke suala la umaarufu pembeni.

Comments are closed.