The House of Favourite Newspapers

Tuache Siasa Kwenye Sakata la Yondani na Kwasi

MECHI ya watani imechezwa wikiendi iliyopita, Simba ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga, mchezo ukichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ni mechi kubwa ambayo ilikuwa na msisimko wa aina yake na ambayo mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania walikuwa wakiifuatilia kutokana na historia na umuhimu wake kwa mustakabali wa soka letu.

 

Moja ya tukio lililoibuka kwenye mchezo ule ni tuhuma za nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani kumtemea mate kiraka wa Simba, Asante Kwasi.

Tukio hilo limenaswa na kamera za Azam Tv ambao ndiyo wenye haki za kurusha matangazo ya michuano hiyo ya Ligi Kuu Bara. Ingawa mwamuzi hakuliona tukio hilo lakini kamera hizo zilimuonyesha mlalamikaji ambaye ni Kwasi akionyesha anachodai kufanyiwa na Yondani wakati mchezo huo ukiendelea lakini bado mamlaka husika hazijatoa ufafanuzi.

 

Baada ya mchezo huo kumekuwa na tafsiri nyingi kuhusiana na tukio hilo huku asilimia kubwa zikionekana kuegemea zaidi kwenye ushabiki wa Simba na Yanga na kukwepa ukweli ama kwa makusudi kabisa au kwa kutokujua nini athari zake. Baadhi ya wadau wa Yanga wanatoa vielelezo mbalimbali vya nyuma kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha hata wachezaji wao walishafanyiwa ambacho Yondani alidaiwa kukifanya juzi na hakuna yeyote aliyeibuka kukemea.

 

Ingawa hata hivyo vielelezo vya matukio hayo ya nyuma havijitoshelezi. Wanatumia utetezi kama hoja kwamba alichokifanya Yondani ni kitu cha kawaida kwenye michezo jambo ambalo si la kiungwana. Msisitizo wetu ni kwamba tusithubutu kusimama kutetea kosa kwa kutumia kosa jingine.


Tuwasaidie wachezaji wetu wakue na waondokane na vitendo ambavyo si vya kiungwana kwenye michezo. Hiyo ndiyo namna ambayo tunaweza kuwajenga na kukuza soka letu kuanzia kwenye ngazi ya klabu mpaka timu ya Taifa. Maoni yetu Spoti Xtra ni kwamba alichokifanya Yondani bado ni tuhuma lakini kamati husika zikithibitisha kwamba ni kosa kwa mujibu wa vielelezo lazima awajibike ili iwe funzo kwa wengine. Isifike sehemu tuingize ushabiki kwenye mambo ya msingi kama haya yanayohusu maendeleo ya soka letu. Tuwasaidie wachezaji wetu kwa maslahi mapana bila kuangalia huyu ni klabu gani au rangi gani.

 

Yondani au mchezaji mwingine yeyote akienda kufanya kitendo kama kile nje ya nchi ni aibu kubwa kwa Taifa, hivyo ni busara mambo kama yale yakakemewa kwenye ngazi ya chini kabisa kabla ya kufika mbali. Lakini vilevile tunaamini kwa klabu yenye umri wa Yanga mpaka sasa ilipaswa kuwa imeshajiridhisha na kile kilichotokea dhidi ya mwajiriwa wao na kuchukua hatua za ndani badala ya kukaa tu na kuchukulia kama ni jambo la kawaida.

 

Wao ndiyo walipaswa mpaka sasa kuwa wameshathibitisha kuwa kile kilichotokea ni kweli au si kweli na kusafisha jina la klabu dhidi ya mambo ambayo yamekuwa yakienea kwenye mitandao ya kijamii. Tubadilike tuache ukweli uitwe ukweli, tusifunike mambo kwa mwavuli wa kishabiki.

 

Tuangalie mambo kwa maslahi mapana ya soka la Tanzania, tusilee makosa kwa sababu za kishabiki kila kitu kifanyike kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

BODI YA UHARIRI, SPOTI XTRA

Comments are closed.