The House of Favourite Newspapers

Tatizo Kubwa Linaloitafuna Yanga ni Uongozi

YANGA imeanza kinyonge mechi zake za makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kupoteza ugenini dhidi ya USM Algiers. Ni moja kati ya mechi ngumu ambazo wadau wa soka wamekuwa wakinukuliwa wakiilaumu Yanga kwa jinsi walivyoiingia kwa mikakati dhaifu ikiwemo ukosefu wa wachezaji wake nyota ambao inaelezwa wengine walikuwa kwenye mgomo.

 

Yanga waliingia kwenye mechi hiyo bila wachezaji wake wengi ambao ni kama uti wa mgongo. Lakini bado wana mechi tano kwenye hatua hiyo ya makundi ambazo wanaweza kufanya vizuri na kusonga mbele katika michuano hiyo. Lakini tatizo tunaloliona kwa Yanga lipo kwa uongozi.

 

Ni udhaifu mkubwa kwa timu kubwa kama Yanga kukosa hata kikao cha mpangilio wa michuano ya Kombe la Shirikisho.

 

Sababu waliyoitoa Yanga ni kwamba walikosa viza wakati wa harakati za kwenda kwenye mkutano huo ambao ulifanyika kabla mashindano hayo kuanza. Tunachohoji ni kwamba kwani kikao hicho kilikuwa dharura? Kwa nini Yanga tu ndiyo iliyokosa viza ya kuingia Misri? Hiyo ni dalili kwamba kuna sehemu kwenye uongozi wa Yanga kuna tatizo na wanapaswa kujipanga upya au kuangalia jinsi wanavyofanya mambo yao.

 

Mambo kama haya si ya kufanya kwenye mashindano makubwa kama hayo, ni vitendo vya aibu kwa nchi kufanya mambo kwa mazoea.

 

Matokeo yake mpaka Yanga inakwenda Algeria kwenye mchezo wa kwanza hawakujua ni nini kilizungumzwa katika kile kikao na hata CAF haikujua kuwa klabu hiyo mdhamini wake ni nani na mambo mengine mengi ya msingi ambayo yanapaswa kuwasilishwa awali kutokana na haki za matangazo ya televisheni. Ndio maana Yanga wakaishia kuambiwa wazibe nembo la SportPesa kwavile wenye haki za televisheni walikuwa hawaelewi na walikuwa hawajajulishwa kwenye vikao rasmi.

 

Matokeo yake Yanga wakaishia kuhatarisha udhamini wao kwasababu ambazo ukiangalia chanzo chake unaona ni kwenye uongozi wenyewe, hayo ni makosa ya kimkakati ambayo yanaonyesha kwamba kuna tatizo kwenye mpangilio wa shughuli za kila siku na matukio ya klabu. Shukrani kwamba wiki iliyopita, CAF wameelewa na kuwaruhusu kuendelea kutumia vifaa vya
mdhamini wao.

 

Maoni yetu ni kwamba viongozi wa Yanga watulie na wafanye kazi zao kiufanisi zaidi kwa masilahi ya klabu na watambue majukumu yao ni nini, waache kufanya mambo kwa mazoea. Wafanye mambo kadri ya umuhimu wake na watu wenye uwezo sahihi wakae kwenye nafasi sahihi na wawe na kalenda ya mambo mbalimbali ili kuepuka mkanganyiko.

 

Lakini vilevile ifike mahali kama mambo hayaendi sawa washirikishe wenye timu yao kwa mujibu wa katiba zao, ambao ni wanachama. Viongozi wasisubiri mpaka mambo yaende mrama ndipo wakae mezani na wanachama. Kuna umuhimu pia wa kujaza nafasi zilizowazi ikiwemo ile ya mwenyekiti aliyebwaga manyanga, Yusuf Manji.

 

Hakuna haja ya kuendelea kuacha kivuli wakati timu inataabika. Kupatikana kwa viongozi kwenye nafasi zilizo wazi kunamaanisha kwamba kutakuwepo na mawazo mapya na mtiririko wa utendaji wa kila siku utakuwa umeboreshwa zaidi ya ilivyo sasa ambapo kunatokea makosa ambayo yanaonyesha kabisa kuna sehemu kuna shida kwenye utendaji.

Comments are closed.