NIANZE kutoa kongole kwa Mbwana Samatta na Ally Salehe Kiba ‘King Kiba’ kwa kile ambacho walikifanya mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kutumia vipawa vyao kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya elimu hapa nchini.
Kwangu ni wazo zuri ambalo linatakiwa kuungwa mkono pale litakapokuja kufanyika kwa mara ya pili kwani tumeona ushiriki wa watu kwa kiasi fulani haukuwa mkubwa kama ilivyotarajiwa.
Lakini pia nitoe rai kwa mastaa wengine kuiga na kufanya kama vile au zaidi na walivyofanya Kiba na Samatta kwa kuchangia kidogo kwa kile ambacho wanakipata kutoka kwa jamii ambayo inawasapoti.
Baada ya hapo sasa nageukia kweye kile ambacho ndicho kimenifanya nishike kalamu na kuandika makala haya. Wikiendi iliyopita pale Kenya kulikuwa na fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup ambapo Simba ilipambana na Gor Mahia.
Baada ya dakika 90, Simba walijikuta wakipewa kipigo cha mabao 2-0 na kombe hilo kutua tena kwa Gor Mahia ambao mara ya kwanza walilichukua hapa jijini Dar mwaka jana, hivyo wamejipatia nafasi ya kwenda kucheza mechi ya kirafiki na Everton nchini England.
Kikubwa siyo kwamba tumepoteza nafasi ya kwenda kucheza na Everton katika Uwanja wa Goodson Park, bali ni mazingira ya ushiriki kwa timu zetu.
Ukiangalia mwanzo mpaka mwisho kwa jinsi ya timu zetu zilivyoshiriki ni kama hazikuwa na maandalizi mazuri kwani mwanzoni tu Yanga walivurumishwa katika michuano hii kwa kufungwa na Kakamega Home Boys. Baadaye JKU ya Zanzibar nayo ikatolewa kwa kufungwa na Gor Mahia.
Wawakilishi wetu wengine, Singida United na Simba nao hawakuwa na matokeo ya kuridhisha licha ya kwamba ndiyo wameshika nafasi ya tatu na pili. Katika mechi zote tatu walizocheza, Singida United hawakufanikiwa kupata ushindi ndani ya dakika 90 zaidi ya kubebwa na penalti hadi wanakamata nafasi hiyo ya tatu.
Ukija kwa Simba, wao nao licha ya kwamba ndiyo walicheza fainali na Gor Mahia, lakini katika dakika 270 ambazo ni sawa na mechi tatu walizocheza, hawakufanikiwa hata kufunga bao moja ndani ya muda huo. Walikuwa wanasonga mbele kwa mikwaju ya penalti.
Jambo hilo linonyesha kwamba jinsi ya timu zetu zilivyo pamoja na mfumo mzima wa ligi yetu inavyokwenda.
Inashangaza sana kuona bingwa wa nchi anakwenda kwenye michuano halafu anamaliza mechi tatu bila hata kupata bao.
Sidhani kama kwa mwendo huu tunaweza kuwa na matumaini ya kuona timu zetu zikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nadhani kwa kupitia michuano hiyo ya SportPesa iwe fundisho kubwa kwetu kuona kwamba tunatakiwa kubadilisha juu ya mwenendo wetu na kuboresha baadhi ya mambo kuona tunatoka kwenye tope ambalo tumekwama sasa na kwenda mbele zaidi kama tunataka kuona timu zetu zinapata mafanikio kwenye ngazi za klabu hasa kwa upande wa kimataifa.
Tunatakiwa kuangalia matokeo waliyoyapata Simba, Yanga, JKU na Singida United kwenye michuano hiyo, kisha tuyafanyie kazi kweli kwa ajili ya kuzijenga timu zetu ili hata ikitokea kwa wakati mwingine michuano hii inatokea basi tufanye vizuri.
Comments are closed.