The House of Favourite Newspapers

Ndemla: Nasaini Yanga Mazembe

Said Hamisi Ndemla

KIUNGO fundi anayesugua benchi Simba, Said Hamisi Ndemla juzi usiku alikutana na Yanga jijini Dar es Salaam na kuwahakikishia kwamba siyo anabipu ni kweli yuko tayari kusaini kama wakikubaliana na ofa yake yenye masharti mawili.

 

Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita Simba walikuwa wakimuingiza kipindi cha pili na kubadilisha kabisa upepo wa mchezo, amewaambia Yanga kwamba wampe Sh.milioni 80 tu asaini lakini pia awepo kwenye kikosi cha kwanza.

 

Lakini Ndemla akawaambia viongozi hao ukweli kwamba hata Simba amezu-ngumza nao na kuwataka wampe Sh.milioni 70 pamoja na mkataba wake uwe pia na sharti la kuwemo kwenye kikosi cha kwanza wakikubaliana nae atabaki Msimbazi.

 

Habari zinasema kwamba Ndemla amewaambia Yanga kwamba dau la Simba ni dogo kwavile amekuwa nao muda mrefu na kilichokuwa kinacho-mkimbiza ni kusugua benchi.

 

Ndemla aliibuliwa kwenye kikosi cha vijana cha Simbamba na mastaa wengine kama Jonas Mkude, Ramadhani Singano (Azam FC) Hassan Isihaka (Mtibwa Sugar) na Miraji Athuman wa Singida United.

 

Akizungumzia na Spoti Xtra jana Jumamosi jijini Dar es Salaam, Ndemla alisema; “Nimekutana na Yanga nimewapa ofa yangu, nasubiri uamuzi wao.”

 

“Yanga wao wameshaonyesha wazi kunitaka kwa hali na mali kwani nimekuwa nikiongea nao mara kwa mara, nimewatajia ofa yangu ya Shilingi milioni 80 na wameniambia ngoja wajadiliane hivyo wakirudi na ofa yangu mkononi nadhani hata leo nitakuwa tayari kuvaa uzi wa njano kwani maisha ni popote,” alisema Ndemla ambaye Simba wamepanga kumpeleka kwa Mohammed Dewji ‘MO’ akamalizane nae.

 

Dau analotaka Ndemla Yanga ndilo Simba wanalodaiwa kumpa straika Shiza Kichuya ingawa inadaiwa bado hajasaini rasmi Msimbazi kuna vitu wanakamilisha.

Vigogo wa Simba wanajua kwamba wakimkutanisha mchezaji huyo uso kwa uso na MO hachomoi na atasaini kiulaini kabisa kuliko anavyowachezea akili wao.

 

“Simba nimewapa masharti kama yatakubalika basi nitaendelea maana nimeichezea muda mrefu. Nahitaji kupewa kipaumbele cha kucheza tofauti na ilivyokuwa hapo awali,”alisema Ndemla ambaye kabla msimu haujamalizika alihusishwa na timu moja ya Sweden.

 

“Hakuna ubishi kuwa Simba ndiyo utambulisho wangu na ndiyo maana siangalii sana suala la fedha kusaini zaidi naangalia zaidi nafasi yangu kwenye kikosi hivyo, nimewaambia kabla sijaongeza mkataba basi viongozi wanihakikishie kucheza kwanza katika kila mchezo nitakapokuwa mzima, wakiridhia hilo nasaini,”aliongeza Ndemla ambaye anatembelea gari aina ya Toyota Raum New Model.

 

Usajili wa timu za Ligi Kuu Bara umeanza rasmi juzi Ijumaa ingawa Yanga inaonekana kwenda mwendo wa kuchechemea kutokana na sababu za kiuchumi.

Comments are closed.