RUBY BAND &THE MAFIK BAND, BENDI BONGO FLEVA TISHIO
ILIPOIBUKA Yamoto Band mashabiki wengi waliona mapinduzi ya Muziki wa Bongo Fleva kupitia bendi yamefika. Ni kweli Yamoto Band ikiwa na vichwa vinne, Maromboso, Becka Flavour, Enock Bella na Aslay ilisumbua katika muziki huo huku ikifanikiwa kutoa vibao vikali sambamba na kupata shoo kibao ndani na nje ya nchi.
Sio hivyo tu, Yamoto Band ndiyo bendi ya kwanza kutokea kwenye Muziki wa Bongo Fleva ikiwa imeweka historia kibao ya ‘kuzurura’ kwenye majukwaa mengi ya siasa katika kampeni pamoja na sherehe mbalimbali za kitaifa.
Ukiachana na hilo, zipo bendi zilizoibuka lakini zikaambulia za uso kama vile Skylight Band na nyingine nyingi. Kwa sasa zimeibuka bendi mbili za Muziki wa Bongo Fleva zinazokimbiza kwa kasi ambazo ni Ruby Band pamoja na The Mafik.
Over Ze Weekend limefanikiwa kuzipata bendi hizo na kuzifanyia mahojiano moja kwa moja, hizi hapa zisikie;
RUBY BAND
Over Ze Weekend: Mashabiki wangependa kujua bendi yenu ina wasanii wangapi?
Ruby Band: Bendi ina wasanii wa kuimba wawili ambao ni C Minor pamoja na Kwela TZ. Ukiunganisha kuanzia wapiga drums, madansa na watu wengine wa vocal jumla tupo 12.
Over Ze Weekend: Tumeona bendi nyingi zinakuja kwa kasi na kupotea, vipi kwa upande wenu?
Ruby Band: Kuna kitu ambacho tumekiunda sisi kama sisi cha ushirikiano kwa kila mmoja. Tulipoanza waimbaji tulikuwa wanne lakini kutokana na tabia mbovu kundini wawili walifukuzwa na sasa waimbaji tumebaki wawili ambao tunajielewa.
Over Ze Weekend: Nani anayewatungia na mpaka sasa mna ngoma ngapi?
Ruby Band: Kwa sasa tuna Ngoma ya Kuntu tuliofanya kwa C9 Kanjenje. Ngoma nyingi tulizofanya zamani tukiwa wanne hatuwezi kuzitumia. Kuhusu kutunga huwa tunatunga wenyewe wakati mwingine tukishirikiana na uongozi.
Over Ze Weekend: Mlishawahi kufikiria kuwaongeza wasanii wa kike kwenye bendi yenu?
Ruby Band: Hilo limekaa kiungozi zaidi, kwa sasa tunafikiria tusonge tukiwa wawili kwanza.
Over Ze Weekend: Mnapiga ‘live band’ au ndio wale wa kuiga CD kwa nyuma?
Ruby Band: Tuna uwezo mkubwa wa kuchanganya, tunapiga kuanzia akapela, live band mpaka playback inategemea shoo tunaopiga.
Over Ze Weekend: Asanteni sana.
THE MAFIK
Over Ze Weekend: Nani aliwapa wazo la kuita bendi yenu The Mafik?
The Mafik: Wazo lilitoka kwa uongozi ambao ulikuwa unasimamia Club ya Cube ambayo kila Jumapili walikuwa wanaalika wasanii kwa ajili ya kupafomu ‘Extreme Sunday’ kuna baadhi ya wasanii ambao walikuwa tayari wapo na wanafanyakazi hapo kama vile Enock, Mbalamwezi na wadada wengine wawili kwa hiyo hao walikuwa hapo ‘Official’ kama wanamuziki wa bendi ya hapo.
Over Ze Weekend: Nini maana ya The Mafik?
The Mafik: Mafik ni neno la Kikongo linalimaanisha Bahati kwa hiyo The Mafik naweza nikasema tumebahatika na ili uwe na bahati ni lazima ubarikiwe kwa hiyo sisi tumebarikiwa.
Over Ze Weekend: Mna menejimenti?
The Mafik: Yeah, tunayo.
Over Ze Weekend: Mnasimamiwa na nani?
The Mafik: Tupo chini ya King Empire.
Over Ze Weekend: Mna nyimbo ngapi?
The Mafik: Zipo nyingi tu ambazo hazijatoka kama 20 ila ambazo tumeziachia tayari ni tatu, ambayo ni Passenger, Carola na Sheba.
Over Ze Weekend: Ni mafanikio yapi ambayo mmeyapata?
The Mafik: Makubwa sana kwa sababu Passenger ni wimbo ambao umeweza kupokelewa kwa ukubwa sana ukizingatia ni wimbo wetu wa kwanza lakini umepokelewa kwa ukubwa sana na siwezi nikasema ni mafanikio gani ila mafanikio ni mengi hadi kualikwa kwenye matamasha makubwa kama South Africa kwenda kufanya performance.
Over Ze Weekend: Nani huwa anawatungia nyimbo?
The Mafik: Tunaandika wenyewe na wote ni waandishi wazuri lakini hatuzuii mtu yeyote mwenye idea ya wimbo kutubariki tuimbe tunawakaribisha sana.
Over Ze Weekend: Majina yenu wote kwa usahihi?
The Mafik: Mimi naitwa Hamadi Hassan lakini jina la muziki ni Hamadai, kuna Mbalamwezi anaitwa Abdallah Yusuph na Rhino anaitwa Salehe Kheri.
Over Ze Weekend: Asanteni sana.
The Mafik: Karibu!
Story:SHAMUMA AWADHI
Comments are closed.