Simba Yaanika Silaha Tatu Mpyaaa

Meddie Kagere (kulia)

 

KLABU ya Simba, jana Alhamisi ilitambulisha silaha zake tatu mpya ambazo zimejiunga na timu hiyo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya usajili wa kikosi hicho.

 

Simba iliwatambulisha wachezaji Meddie Kagere, Pascal Serge Wawa na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao wamejiunga na timu hiyo kwa kuichezea msimu wa 2018/19.

 

Kagere ametua Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya, Dida aliyekuwa Afrika Kusini na Wawa ambaye alikuwa mchezaji huru akitokea El Merreikh ya Sudan.

Pascal Serge Wawa (kulia).

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wachezaji hao, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema usajili wa nyota huo umetokana na mapendekezo ya benchi lao la ufundi ambapo lilihitaji wachezaji wa namna hiyo kutokana na msimu ujao kuwa na mashindano mengi.

 

“Usajili huu tulioufanya umetokana na pendekezo la kocha ambalo yeye ndiye ametaka wachezaji wa namna hii wawepo ndani ya kikosi kwa ajili ya kuifanya timu ifikie kile ambacho imekipanga.

 

“Watu wanahoji juu ya kuongeza kipa mpya lakini niwaambie kwamba wao makocha ndiyo walitaka kipa Aishi Manula awe na mbadala wake, Dida limekuwa chaguo zaidi kwa sababu hakuna kipa wa hapa ndani ambaye amecheza michuano mikubwa zaidi kumpita yeye, ndiyo maana amerejea tena ndani ya timu.

 

“Kwa Kagere sote tunaona msimu uliopita jinsi ambavyo timu ilikuwa inahangaika kupata matokeo wakati ambao tukiwakosa Emmanuel Okwi na John Bocco, hivyo tulimhitaji mtu wa namna yake kwa ajili ya kuwasaidia katika mechi zetu na kwake hakuna ubishi anaweza kufanya hivyo kwa sababu hata mara ya mwisho alitufunga katika SportPesa. Hata kwa Pascal Wawa naye ni hivyohivyo.

 

“Lakini tumemchua Wawa kwa sababu anakuja kuchukua nafasi ya beki wetu Juuko Murshid ambaye yeye anafanya majaribio kwenye kikosi cha SuperSport cha Afrika Kusini,” alisema Manara.

 

Aidha, Manara aliongeza kwa kusema: “Hapa siyo mwisho, tutaendelea kusajili nyota wengine ambao tutaona wanahitajika, hadi sasa ndani ya timu wameondoka Laudit Mavugo na Juuko Murshid.”

Kipa wa zamani wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ (kulia).

 

Daktari asema wapo safi

Katika hatua nyingine, Daktari wa Simba, Yassin Gembe amesema wachezaji hao waliosajiliwa wapo vizuri katika suala la afya zao baada ya kufuzu vipimo mbalimbali ambavyo walifanyiwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo ya Muhimbili.

 

Gembe ameongeza kuwa kikosi hicho kitawakosa wachezaji kadhaa ambao wana majeraha ya aina mbalimbali huku wakihitaji pia kupumzika.

 

Wachezaji hao ni pamoja na Shiza Kichuya, Jonas Mkude, John Bocco, Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi, Shomari Kaombe, Aishi

 

 

Manula na Haruna Niyonzima ambapo wachezaji wote hao watakuwepo wakati wa kujiandaa na msimu mpya ‘pre season’.

Beki Salim Mbonde ana majeraha makubwa ambayo yatamlazimisha kuwa nje kwa kipindi kirefu zaidi.

 

Mrundi awafurahia Kagere, Wawa

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma raia wa Burundi akizungumzia juu ya wachezaji hao alisema: “Hawa ni aina ya wachezaji ambao tulikuwa tunawataka ndani ya timu kwa sababu hawafanyi makosa sana wakiwa uwanjani kama ambavyo sisi tulikuwa tunataka.

“Watu wanasema nyota hawa ni wazee lakini mimi niwaambie hawa ni wazee wa kazi na timu haiwezi kuwa na vijana au wazee peke yake lazima kuwepo na mchanganyiko.

 

Agusia mipango Kagame Cup

Kocha huyo akigusia pia mipango yake juu ya Kombe la Kagame ambalo linaanza leo, alisema: “Kombe hili tutatumia zaidi wachezaji wale ambao hawakuwa na nafasi ya kucheza katika ligi sambamba na nyota hawa wageni ambao wamekuja, pia nilizuia juu ya wachezaji kuachwa kiholela kwa kutaka wapewe nafasi katika kombe hili,” alisema Djuma.

 

Meneja afunguka Yanga walimfuata Kagere

Meneja wa straika Meddie Kagere, Patrick Gakumba amesema kwamba kabla ya mteja wake kusaini Simba alifuatwa na watu wa Yanga ambao walikaa hoteli moja nchini Rwanda lakini yeye aligoma kuwauzia na kusisitiza mshambuliaji huyo anakwenda Simba.

 

‘Dida’ afunguka

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Dida ambaye ni kipa wa zamani wa Yanga, alisema: “Namshukuru Mungu kwa kutambulishwa kuwa mchezaji wa Simba lakini kubwa nashukuru kwa thamani niliyoonyeshwa na viongozi, nina uwezo na ninachowaomba kwa sasa mashabiki, viongozi na makocha tuwe pamoja.”

 

Meddie Kagere anena

“Ninawashukuru wote waliofanikisha mimi kuwepo hapa akiwemo meneja wangu ambaye ndiye aliyekuwa mtu wa kati hadi dili linakamilika.

 

“Simba ni timu kubwa, lazima nionyeshe uwezo, nipo kwa ajili ya kufanya kazi ambayo watu wanataka kufanya, kama mshambuliaji ninatakiwa kuonyesha uwezo uwanjani, nitafanya kazi yangu ile inavyotakiwa.”

 

Pascal Wawa huyu hapa

“Ninafurahia kurudi Tanzania tena kwa mara nyingine, ninawashukuru viongozi wa Simba kwa mkataba walionipa, mimi sitaongea sana ila nitaonyesha kazi yangu uwanjani ndiyo itazungumza na kuonyesha ni namna gani ya beki nilivyo kama ni mkubwa au la.”

Loading...

Toa comment