The House of Favourite Newspapers

Yondani Anastahili Heshima Badala Ya Kejeli Mnazompa!

Beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani

 

NIMESIKIA beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani amekuwa katika mazungumzo na klabu yake tayari kwa ajili kuongeza mkataba mwingine.

Achana na zile taarifa zilizoandikwa na magazeti (si Championi) kwamba ameishajiunga na Simba kwa miaka miwili. Simba tayari walilieleza Championi kuwa kwa msimu ujao, hawakuwahi kuwa na pendekezo la Yondani.

 

Walieleza wazi kwamba kama wangemtaka Yondani, basi wangemsajili mapema sana kwa kuwa Yanga ilishinda kumpa mkataba mpya kwa muda mwafaka kwa kuwa alimaliza mkataba muda mrefu sana.

 

Wakati fulani, niliwahi kuandika nikimsihi Yondani kuitumikia Yanga hadi hapo watakapokubaliana. Niliamini alitakiwa kufanya vile na kuisaidia Yanga hadi hapo watakapofikia mwafaka.

 

Hata hivyo, tunarudi upande wa Yondani kwamba naye kama mwanadamu anachoka. Lazima tujue ana familia na ana wazazi wake pia wanamtegemea.

Unajua, Yondani amekuwa mvumilivu na unaweza kusema amejitahidi. Sote tunakubali anapoitumikia Yanga anajituma kwa kiwango cha juu kabisa na watu wote wamekuwa wakimpongeza kwa kazi nzuri.

 

Sasa kitendo kinachofanyika sasa kumvurumishia matusi mtandaoni baada ya zile taarifa za uzushi kwamba amesaini Simba, nafikiri si sahihi hata kama zingekuwa na ukweli.

 

Kuichezea Yanga si lazima, uamuzi wa mchezaji mwenyewe kwa kuwa mpira kwake ni kazi. Bahati mbaya sana, Yondani hajachukua uamuzi kabla ya kuonyesha uvumilivu, kilichotokea ni viongozi kuahidi kwamba wangemtimizia ahadi kwa kumpa fedha wakati fulani, lakini haikuwa hivyo.

 

Hapa si kwamba nawalaumu viongozi, natambua nao wako katika hali ngumu na wanaendelea kupambana kuhakikisha mambo yanakwenda sawa ingawa nimekuwa nikihimiza suala la umoja na ubunifu kitaalamu kufanikisha mambo.

 

Wale wanaomtukana Yondani ninaamini wengine wanakuwa ni watu wa makundi haya mawili. Inawezekana hawana familia na wanaishi nyumbani kwao au ni watu ambao wana familia lakini bado hawajaelewa maana ya kazi hasa ni jambo lipi.

 

Katika kundi hili la kwanza, hawa watu hushindwa kuelewa kwamba anayekuwa ofisini hutaka kupata maslahi ofisini kwake kama ambavyo mjomba wake (kama anakaa kwa mjomba), anavyopambana kupata fedha za kuendesha familia akiwemo yeye.

 

Yondani ana familia, lazima awe na kipato k i t a k a c h omu w e z e s h a kuiendesha familia yake. Hivyo suala la kuhakikisha analipwa vizuri wala si mjadala tena.

 

Kundi la pili ni lile ambalo huona mwanasoka ni mtu anayejifurahisha au mtu anayetoa msaada tu. Wako wanaona mwanasoka ni mtu anayepaswa kucheza tu lakini hakuna shabiki anayepigania maslahi yake anaposikia hajalipwa.

Iko haja ya kujifunza kwamba wanasoka nao ni wanadamu wanahitaji maslahi yao ili kuendeleza maisha yao. Hakuna upendo wa kutoka upande mmoja uliopdumu milele.

 

Mara kadhaa nimeandika makala kuwasihi wachezaji wa Yanga kuwa na subira ili kuisaidia timu yao. Lakini najua na ndiyo maana leo nimeandika kwamba nao ni binadamu na wana mahitaji yao. Hivyo kama kuna sehemu wamefanya uvumilivu, wakati mwingine pia wanachoka.

 

Hivyo si sahihi kumtukana Yondani kwa kuwa kuna taarifa kaenda Simba, ambazo si kweli. Si sahihi kumvurumishia maneno makali na machafu eti kwa kuwa amegomea kuichezea Yanga.

 

Inawezekana ikawa vizuri kufikisha ujumbe kwa viongozi wa Yanga kuwaambia wampe Yondani anachohitaji na kama ni kikubwa, wafanye juhudi za kumpata na kuzungumza naye ili kumalizana naye kama walivyoanza kufanya.

Yondani kaifanyia Yanga mambo mengi sana, huenda maumivu ya upendo wake kwa Yanga ni makubwa sana hata kuliko yule anayetukana akitaka watu wamuone.

 

Si kila mwenye nafasi ya kuwa na akaunti ya mtandao wa kijamii anaweza kutukana na kusema watu hovyo. Mjifunze, badilikeni na acheni umbumbu wa mitandao ya kijamii.

Comments are closed.