The House of Favourite Newspapers

Sanga Ni Wakati Wa Kuiacha Yanga Kwa Wengine

Clement Sanga.

 

NI dhahiri kuwa mzigo wa kuiendesha Yanga umekuwa mzito kwa Clement Sanga, hivyo ni wakati wa kuiacha klabu hiyo kwa wengine.

 

Sanga ambaye ni makamu mwenyekiti klabuni hapo, pia amekuwa akikaimu uenyekiti wa Yanga kwa muda mrefu baada ya mwenyekiti wao, Yusuf Manji kujiondoa, anaonekana kuelemewa na klabu hiyo kongwe nchini.

 

Ukiondoa wakati mgumu ambao Yanga wanapitia wa mgogoro wa kiuchumi, lakini pia inaonekana hali si shwari ndani yake na Sanga ameshindwa kuifanya kuwa pamoja.

 

Timu haifanyi vizuri, morali ya wachezaji imeshuka, lakini pia wanachama hawako pamoja, kila mtu anasononeka kivyake huku Sanga ambaye kama tegemeo, hazungumzi kitu, yuko kimya kama mambo yako sawa.

 

Kocha wa Yanga, Mcongomani Mwinyi Zahera mpaka sasa hana kibali cha kufanyia kazi, sekretarieti ya Yanga chini ya Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa inaonekana kusambaratika, lakini Sanga yuko kimya kama hakuna linaloendelea.

 

Huu sasa ulikuwa wakati mwafaka kwa Sanga kuachia ngazi na kuwapisha wengine kuliendesha gurudumu la Yanga. Mzigo unaonekana mzito na umemuelemea.

 

Wakati mwingine ni vizuri kuondoka mwenyewe pale unapoona mambo magumu ili wengine wakusaidie.

Wanayanga hawana furaha tena, timu yao kila ikiingia kwenye mechi sasa ni vipigo, wachezaji tegemeo hawaonekani na wale waliopo hawajitumi kabisa.

Wanayanga wanaonekana wamekata tamaa kabisa wakati msimu wa Ligi Kuu ya Bara ukitarajia kuanza mwezi ujao. Unajiuliza bado Sanga anabaki Yanga kwa nini?

 

Kwa nini asiwapishe wengine waendeleze pale walipoishia. Inawezekana Sanga anaipenda sana Yanga, lakini kwa ilipofikia awaachie mashabiki na wanachama wa timu hiyo ili waangalie namna ya kufanya ili kuiokoa timu yao.

Imekuwa ni aibu kwa klabu kubwa kama Yanga, leo unasikia bado wachezaji wana madai kibao. Usajili wao wenyewe kwa msimu ujao haueleweki huku ikiamua pia kurejesha wachezaji wa zamani. Huku ni kuanguka kwa Yanga kabisa.

 

Sanga asisubiri mpaka atimuliwe, angejiweka kando wenye Yanga yao wengine wajipange upya.

Ukiangalia timu tangu imeingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika bado inasuasua na ipo mkiani kwenye kundi lake baada ya kucheza mechi tatu na haijafanikiwa kushinda zaidi ya kuambulia sare moja.

 

Yanga ambayo ilitinga pia kibahati bahati, mpaka sasa jumla imefungwa mabao nane baada ya juzi pia kuchapwa mabao 4-0 na Gor Mahia, awali ilitoka sare na Rayon Sports mechi ikipigwa jijini Dar, pia ikapigwa mechi yake ya kwanza na USM Alger kwa mabao 4-0.

 

Ukiangalia matokeo hayo utabaini kuwa kuna kitu kikubwa kinaonekana kuwa nyuma ya pazia, kwa nini timu haijapata ushindi kwenye michezo mitatu?

 

Wachezaji wana nini hadi waruhusu hivi, ni wakati wa waliopo madarakani kujitafakari kwani hivi vipigo vinavyoendelea kuna walakini, ni lazima timu ibadilike haraka sana kabla ligi haijaanza.

 

Kama mambo yataendelea hivi basi kuna rekodi mbaya ambayo Yanga wataandika kwenye michuano ya mwaka huu. Hatua za haraka zichukuliwe kuiokoa timu.

Comments are closed.