The House of Favourite Newspapers

Huyu Makambo wa Yanga Ni Noma

MASHABIKI wa Yanga hawajabahatika kuona mavitu ya straika wao mpya, Heritier Makambo lakini Juma Abdul na Amissi Tambwe wamewahakikishia jamaa anajua.

 

Wachezaji hao wamemfananisha straika huyo na Mzimbabwe Donald Ngoma alivyotua Yanga kipindi kile kwa jinsi alivyokuwa moto.

 

Makambo ambaye ni raia wa DR Congo aliyejiunga na Yanga akitokea FC Lupopo, ni chaguo la Kocha Mwinyi Zahera ambaye amewahi kutamka kwamba wachezaji wote aliopen-dekeza yeye wasajili wa kigeni uwezo wao ni zaidi ya wale aliowaona Tanzania.

 

Yanga imekuwa ikifanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Polisi Kurasini ambao ni marufuku mashabiki kuingia wala mtu yoyote kupiga picha.

 

“Kwa harakaharaka mtu akiangalia safu yetu ya ushambuliaji anaweza kuidharau lakini ipo vizuri na tunaamini kuwa tutawashangaza wengi. Kuhusiana na Makambo ni bonge la mshambuliaji ambaye naamini atakuwa na msaada mkubwa kwa timu yetu kutokana na uwezo wake,” alisema Tambwe ambaye anaamini msimu ujao ataru di kwenye fomu yake.

 

“Uwezo aliokuwa nao Ngoma kipindi kile anakuja Yanga basi Makambo naye yupo hivyohivyo au anaweza kuwa zaidi, ana uwezo wa kupambana, kutengeneza nafasi lakini pia anajua kufunga, binafsi sina wasiwasi naye,” alisema Amissi Tambwe mmoja kati ya washambuliaji wa timu na ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi klabu hapo kwa wachezaji wa sasa.

 

Naye beki wa kulia wa timu hiyo, Juma Abdul ambaye ni swahiba mkubwa wa Kelvin Yondani alisema kuwa: “Makambo ni mchezaji mzuri na amekuwa akionyesha vitu mazoezini ambavyo vimekuwa vikituvutia wachezaji wengi.”

 

“Kikubwa ni ushirikiano tu, bila ya kufanya hivyo anaweza kuwa mzuri na asiisaidie timu lakini tukishirikiana naye naamini atafanya makubwa,” alisema Abdul ambaye ni miongoni mwa visiki vya Yanga.

 

“Makambo ni mchezaji mzuri na ni chaguo langu kwa hiyo naamini atafanya mambo makubwa, uwepo wake na washambuliaji wengine basi watafanya kitu kizuri kwa msimu ujao,” anasisitiza Zahera ambaye alihitaji wachezaji wengi zaidi wa kigeni wa aina hiyo lakini bajeti ikambana.

 

“Siwezi kusajili straika wa goli 12 kwa msimu, mimi nasajili straika wa zaidi ya goli 20,” alitamba Zahera ambaye ameonyesha uvumilivu mkubwa ndani ya Yanga licha ya misukosuko ya kiuchumi na wachezaji kumgomea mazoezini wakidai stahiki zao.

Makambo ataungana na washambuliaji wengine sita wa Yanga ambao ni Matheo Anthony, Mrisho Ngassa, Tambwe, Ibrahim Ajibu, Yusuph Mhilu na Paul Godfrey.

Comments are closed.