The House of Favourite Newspapers

Kotei Amekosea, Anapaswa Kuchukuliwa Hatua, Hakuna Mjadala

Beki na kiungo kiraka James Kotei.

NILIREJEA kuangalia mechi ya watani wa jadi kati ya Simba dhi­di ya Yanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana.

 

Ilikuwa ni mechi nzuri kwa maana ya burudani ya mch­ezo wa soka kwa kuwa kila upande ulitaka kufanya vizuri.

Ilionekana Simba walikuwa wana nafasi kubwa ya kushin­da mechi hiyo kwa kuwa kiko­si chao kilicheza kwa kiwango kizuri zaidi ya wapinzani wao Yanga.

 

Ukiangalia vizuri, kilichow­aangusha Simba ni aina ya uchezaji, hawakuwa makini hasa katika suala la umaliziaji walipokuwa wakisukuma ma­shambulizi yao kwenda kwa Yanga.

 

Maana katika utengenezaji nafasi, wao walifanya vizuri zaidi, lakini wakakumbwa na ugumu wa umaliziaji. Hata kama kipa Beno Kakolanya alikuwa katika kiwango kizuri, lakini bado suala la kumalizia au umakini katika umaliziaji, haukuwa mzuri hata kidogo.

 

Ukiachana na mchezo kwa jumla, nimeamua niingie ka­tika ule mjadala ambao umeji­tokeza. Hapa ni kuhusiana na mchezaji wa Simba, beki na kiungo kiraka James Kotei.

 

Kotei alionekana akimt­wanga beki wa Yanga, Gadiel Michael, sijui niseme kofi au ngumi, lakini kwa kifupi am­empiga wazi kabisa na si sua­la la kujiuliza mara mbili kama lilitokea au la.

 

Kotei, raia wa Ghana, alikuwa akiwania mpira na Gadiel. Waligongana lakini baada ya hapo aligeuka na kumpiga mwenzake katika ki­wango ambacho katika mch­ezo wa soka hauwezi kusema ni sahihi au bahati mbaya.

 

Alichokifanya Kotei, in­aonekana wazi alikusudia kwa kuwa tu alishikwa na hasira na kushindwa kujidhibiti. Hakuna ubishi, kweli alikuwa na hasira lakini hicho hakiwezi kuwa kigezo cha kusema anapaswa kuachiwa.

 

Nimeona mijadala mingi kuhusiana na hilo, tayari mashabiki wanaona si sawa afungiwe na wengine wa Sim­ba wamekuwa wakisambaza video beki wa Simba, Mo­hammed Zimbwe ‘Tshabalala’ wakiangushana na Vicent Andrew ‘Dante’ na baadaye Dante alitaka kumpiga kichwa lakini akamkosa.

 

Yote hii ni kuonyesha kwamba pia kuna mchezaji wa Yanga alikosea. Ishu hii sasa imegeuka kama vile ushindani wa kuonyeshana makosa.

Pia inawezekana kwa yule atakayeonyesha ukweli au kusisitiza hatua ichukuliwe ataonekana mbaya. Kwa hali yoyote, bila ya kupepesa au chembe ya woga ni hivi; Kotei anapaswa kuadhibiwa.

 

Binafsi namfahamu Kotei kama mmoja wa wachezaji wenye nidhamu sana. Nda­ni na nje ya uwanja, si mtu anayependa makuu, si mko­rofi na mpambanaji.

Unaweza kusema kama mwanadamu alizidiwa hasira lakini yote haya, hayazuii au kubadilisha kwamba alifanya kosa na anastahili adhabu ili kudumisha adhabu na kuten­geneza usawa kwa wengine.

 

Nililivalia njuga suala la Juma Nyosso kumdhalilisha John Bocco. Nilieleza namna tunavyopaswa kuwa na nidha­mu ya juu katika klabu, ndani ya timu na kwenye ligi yetu.

 

Unakumbuka, hata baada ya Asante Kwasi, beki Mgha­na wa Simba kutemewa mate na Kelvin Yondani wa Yanga nilisisitiza suala hili tena kwa msisitizo wa juu.

Nilipata maoni ya watu kad­haa wasiojitambua kwamba nashinikiza Yondani afungiwe. Binafsi bila ya woga, nasisitiza nilitaka aadhibiwe kwa mujibu wa kanuni na si kufungiwa. Kama unakumbuka Yondani alisimamishwa mechi tatu.

 

Leo, bila ya woga hata ki­dogo, msisitizo wangu ni huo­huo kwamba Kotei amefanya jambo la kipuuzi ndani ya mchezo wa soka. Hata kama amekuwa mtu mwema kabla, lakini shambulizi lile kwa Ga­diel, basi anastahili adhabu.

Mpira hauwezi kukubali watu wapigane ngumi. Nime­shangazwa na mwamuzi Jo­nesia Rukya, alionekana wazi aliliona kosa hilo.

 

Hivyo TFF na Bodi ya Ligi, wanapaswa kuchukua hat­ua ili kuwaonyesha wen­gine kuwa suala la nidhamu linapewa kipaumbele na wale ambao wanatetea, basi waji­funze kuweka ushabiki kando na waangalie suala la nidha­mu kama chachu ya kuwapa mafanikio.

NA SALEH ALLY, HOJA YANGU

Comments are closed.