Mkude, Kapombe Wamvuruga Mbelgiji
KUTOKANA na muingiliano wa kimajukumu kwa wachezaji wa Simba ambao wameitwa Taifa Stars, kumemfanya Kocha Mbelgiji Patrick Aussems ashindwe kuwanoa baadhi ya wachezaji wake.
Stars kwa sasa ipo kambini ikijiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Afrika dhidi ya Cape Verde na wachezaji wa Simba ambao wapo kikosini humo, ni Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Aishi Manula na John Bocco.
Simba ambayo katika mchezo uliopita ilitoka suluhu dhidi ya Yanga, leo Jumamosi wataivaa African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar saa moja usiku.
Awali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikubaliana kuwa ligi haitosimama na badala yake wachezaji wangeungana na klabu husika siku moja kabla ya mechi.
Kwa upande wa Simba, wachezaji wao walitakiwa kuripoti kambini juzi Alhamisi jioni ili wakaungane na wenzao, lakini haikuwa hivyo na jana Ijumaa walifanya mazoezi asubuhi na Stars jambo ambalo halikuwafurahisha Simba kutokana na makubaliano kukiukwa.
Aussems alisema awali alikuwa ameandaa program na wachezaji wake wote lakini ilishindikana kutokana na baadhi yao ambao wapo kikosi cha kwanza kuwa na majukumu mengine timu ya taifa.
Kocha huyo alisema suala hilo lilivuruga mipango yake lakini hata hivyo ataiongoza timu hiyo kupata matokeo.
“Wachezaji wako vizuri kwa ajili ya kupambana, na mchezo huu tunahitaji ushindi na siyo kitu kingine, tumerekebisha yale makosa ambayo tulionyesha kwenye mchezo dhidi ya Yanga.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini pia tunahitaji ushindi na katika program zangu nimewakosa baadhi ya wachezaji ambao wapo timu ya Taifa.ingawa niliambiwa watarudi kabla ya mechi, hilo nalo limevuruga mipango yangu kwa kiasi lakini tutapambana kupata matokeo,” alisema Mbelgiji.
Championi Jumamosi lilimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo azungumzie ishu hiyo ambapo alisema: “Kwa sababu wachezaji walikuwa kambi moja tukawataka wafanye mazoezi kwanza na Stars na baadaye wajiunge na klabu yao.”
Timu hizo zimeweka kambi sehemu moja katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach jijini Dar.
MBELGIJI AWAZUIA OKWI, KAGERE
Wakati huohuo, Mratibu wa Simba, Abbas Ally ameweka wazi kuwa Aussems amewazuia nyota wake wa kimataifa walioitwa timu za taifa.
“Hadi sasa hakuna hata mchezaji wetu wa kimataifa aliyeondoka, kutokana na kupata taarifa mapema juu ya uwepo wa mchezo wetu wa kesho dhidi ya African Lyon.
“Kweli baada ya mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya Yanga, kocha aliahidi kuwaruhusu waende kutumikia timu zao za taifa kwani alitegemea ligi ingesimama kupitisha kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars, lakini baadaye aliwazuia baada ya kutangazwa kutosimama kwa ligi hivyo akawataka wabaki hadi wamalize mechi ya kesho (leo),” alisema Abbas
Wachezaji wanaotakiwa kujiunga na timu zao za taifa ni Meddie Kagere na Haruna Niyonzima wote raia wa Rwanda, Juuko Murshid na Emmanuel Okwi wote Uganda huku Clatous Chama akiitwa Zambia.
Comments are closed.