MBELGIJI AMCHUKUA STRAIKA MRUNDI

Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick.

KOCHA Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems amesitisha mipango yake ya usajili wa kiungo mkabaji na badala yake ameomba asajiliwe wachezaji wawili pekee kati ya hao ni beki wa kulia na mshambuliaji pekee.

 

Wachezaji wanaotajwa hadi sasa kutua kwenye usajili wa dirisha dogo ni mshambuliaji Mrundi, Kaleb Bimenyimana beki wa pembeni wa Ivory Coast, Zana Oumar Coulibaly.

 

Awali, kocha huyo alitoa mapendekezo ya kusajili kiungo ambaye alikuwa anatajwa Mkenya, Francis Kahata anayakipiga Gor Mahia, beki wa pembeni, winga na mshambuliaji pekee kabla ya kubadili maamuzi na kuomba asajliwe beki wa kulia na mshambuliaji.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, kocha huyo hataki tena kumsajili kiungo mkabaji kutokana na idadi ya viungo aliokuwa nao katika kikosi chake.

Mtoa taarifa huyo alisema, viungo aliokuwa nao ambao ni Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Claytous Chama, Haruna Niyonzima, Jonas Mkude wanatosha kabisa kuichezea timu hiyo katika ligi na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

“Kocha amesitisha mipango yake ya kumsajili kiungo mkabaji na winga na badala yake ameomba asajiliwe mshambuliaji na beki wa kulia atakayekuwa mbadala wa Kapombe.

 

“Mipango hiyo inakwenda vizuri na wakati wowote beki na mshambuliaji huyo watatua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba baada ya kufikia makubaliano mazuri huku kikibakia ni kupatiwa fedha za usajili pekee.

 

“Beki huyo wa kulia ni Coulibaly ambaye yeye kati ya leo (jana) au leo atatua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba huku tukimsubiria huyo mshambuliaji mpya maalum kwa ajili ya Caf,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Swedy Mkwabi alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Kila kitu kinakwenda vizuri katika usajili wetu baada ya bodi kukutana na kocha na kukabidhi mapendekezo yake.

“Hivi sasa kilichobaki ni utekelezaji pekee kwa kusajili wachezaji hao ambao tutaweka wazi baada ya kukamilika kwa maana ya kusaini mkataba pekee,” alisema Mkwabi ambaye ni mjasiriamali mkubwa mjini Tanga.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Toa comment