The House of Favourite Newspapers

Yanga Waheshimu Mikataba Ya Wachezaji

YANGA ipo kwenye mzozo wa chini kwa chini na mchezaji wake, Beno Kakolanya ambaye amesusia mpaka kucheza.

Siyo Kakolanya tu hata baadhi ya wachezaji wamekuwa wakisusa mara kwa mara kufanya mazoezi na kucheza kama njia ya kushinikiza mikataba yao itekelezwe.

 

Ishu kubwa ambayo imekuwa ikielezwa na wachezaji hao hususani Kakolanya ni kwamba mkataba wake hautekelezwi.

 

Kwa mujibu wa meneja wa Kakolanya ni kwamba Yanga wamelimbikiza kwa zaidi ya miezi mitatu mishahara ya mchezaji huyo na stahiki zake nyingine.

Jambo ambalo linaweza kusababisha akasitisha mkataba wake na timu hiyo ambayo alijiunga nayo akitokea Prisons.

Tatizo la mikataba na stahiki za wachezaji limekuwa likijitokeza mara kwa mara ndani ya Yanga, maoni yetu ni kwamba waangalie njia sahihi ya kumaliza matatizo hayo.

 

Malumbano na wachezaji siyo kitu sahihi haswa kwa taasisi kubwa kama Yanga. Hakuna asiyejua kwamba hali ya uchumi ndani ya klabu za Ligi Kuu kwa sasa ni ngumu kutokana na kukosa udhamini.

 

Lakini kuna namna sahihi ambayo Yanga kama taasisi wanaweza kutumia kutatua matatizo ya wafanyakazi wao ndani kwa ndani bila kuvuja nje na kuanza kuleta maneno ambayo si mazuri.

 

Matatizo ya muajiri na muajiriwa wanayajua wenyewe na kulikuwa na haja ya kukaa na wahusika uso kwa uso na yakamalizwa vizuri zaidi ya kuyaacha yakazidi kuwa makubwa kiasi cha kuleta mpaka mgomo na mizozo ndani ya Yanga.

 

Hapa ndipo tunaposisitiza umuhimu wa klabu kuwa na viongozi imara wanaoelewa majukumu yao. Klabu lazima iwe na uongozi uliokamilika kuanzia juu kwa mwenyekiti mpaka chini kwa wajumbe ili kumuacha Katibu Mkuu afanye mambo ya ndani ya klabu.

Ndio maana TFF na BMT wamekuwa wakisisitiza na kushinikiza Yanga ifanye uchaguzi ili kupata viongozi sahihi watakaoiongoza katika utaratibu unaoeleweka.

 

Haiwezekani kuwa na maendeleo kwenye taasisi kama Yanga bila ya kuwa na viongozi imara na wanaowajibika. Hii ishu ya kuwa na viongozi wa muda kila mara ndio kunaiumiza Yanga kwa vile baadhi yao wanakuwa kama wapita njia, hawawajibiki.

 

Hata suala la kukosa vyanzo mbadala vya fedha inatokana na kutokuwa na uongozi unaoaminika, kwa vile mdhamini hawezi kuingiza fedha yake sehemu ambayo hana imani nayo.

Mdhamini anaingiza fedha yake sehemu ambayo ipo salama, ina mikakati inayoeleweka na haina migogoro wala harufu na mapambano.

 

Ifike mahali Yanga watulize akili wafuate taratibu za kiuongozi lakini wajifunze kwenye suala la mikataba na wawe makini na waheshimu makubaliano na wafanyakazi wao ambao ni kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine.

STORI NA BODI YA UHARIRI -SPOTI XTRA

Comments are closed.