FUNGA KAZI YANGA, BOSI WA USAJILI ATAJA LISTI

LICHA ya kwamba Simba wanawake­jeli kuwa wanasajili kwa mali kauli, lakini Mwenyekiti wa usajili wa Yanga, amesisitiza kuwa funga kazi yao itakuwa ni balaa.

Yanga ambayo haiko vizuri kifedha imepania kufanya mabadiliko kwenye usajili wake kwa kuongeza sura kadhaa za kazi ambazo zitabadili upepo mzun­guko wa pili.

 

Hussein Nyika ambaye ni Mwenyekiti wa usajili wa Yanga, amesisitiza kuwa wako kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa wachezaji wanne pekee ambao ni chaguo lao.

Alisema katika wachezaji hao ambao hatawataja majina wapo wawili wa kigeni na wawili wa ndani.

 

Lakini Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, linajua kwamba wachezaji ambao huenda wakamwaga wino muda wowote ni Reuben Bomba raia wa DR Congo, Kenny Ally (Singida United), Charles Ilamfya (Mwadui FC), Haruna Moshi ‘Boban’ (African Lyon), Eliud Ambokile (Mbeya City) na mshambuliaji Mganda, Umar Kasumba anayekipiga Sofapaka ya nchini Kenya.

 

Nyika alisema, watayaweka wazi majina ya wachezaji hao mara baada ya kumalizana nao akiwemo Ilamfya na Bom­ba ambao wapo jijini Dar es Salaam wakisubiria mikataba yao. Lakini Spoti Xtra linajua kwamba Boban atamalizana na uongozi leo na atatambul­ishwa pale klabuni Jangwani majira ya saa 4 asubuhi.

 

“Hivi sasa tunakamilisha utaratibu wa mwisho pekee ikiwemo kumalizana na klabu zao kama unavyofahamu ni lazima tufuate taratibu zote za usajili na zikikamilika haraka tutawapa mikataba,” alisema Nyika.

 

Akizungumzia usajili wa Boban, bosi huyo wa usajili alisema kuwa “Boban ni mche­zaji mzuri na hata kocha kuna siku alishawahi kumzungumzia kuwa ni mchezaji mtulivu na anayetumia akili na mpira.”

 

“Kila kitu tutakiweka wazi kufikia kesho (leo) kama yeye yupo kati ya hao wache­zaji tuliopanga kuwasajili au vipi,”alisema Nyika.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema “Ninaamini kwamba kama nikiletewa wachezaji ambao nimewap­endekeza wasajiliwe basi tutakuwa vizuri zaidi ya tulipo kwa sasa.”

WILBERT MOLANDI,

 

Loading...

Toa comment