The House of Favourite Newspapers

ZAHERA HARUDI YANGA, CHANZO CHATAJWA

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.

 

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera aliondoka Dar es Salaam wiki hii na unavyosoma hapa mida hii yupo zake Ufaransa. Lakini yameibuka maneno ya hapa na pale kwamba huenda asirudi.

Lakini yeye amewaambia mashabiki kwenye mitandao ya kijamii kwamba atarudi, ingawa bado kuna sintofahamu iliyoibuka baina yake na viongozi.

 

Habari za uhakika kabisa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga ni kwamba Zahera amewaambia watafute tajiri yoyote alipe malimbikizo ya madai ya wachezaji ili kumpunguzia mzigo wa malalamiko, vinginevyo itakuwa ngumu kurejea kwavile anafanya kazi katika mazingira magumu mno.

 

Kocha huyo ambaye amekwenda kwao ‘kusinya’ (kusaini) mikataba ya leseni za biashara zake, viongozi wamedai ana matatizo ya kesi.

 

Habari zinasema kwamba, Zahera amewaambia viongozi wa Yanga kwamba kwavile wameshindwa kusainisha wachezaji wapya, akirudi Jangwani Jumatano ijayo anataka akute wamepata chanzo cha fedha cha kulipa wachezaji wote wanaodai na wawe wamelipwa zote au nusu.

 

Amewaambia kwamba amechoka kuwa msuluhishi wa mambo binafsi ya wachezaji kuhusiana na masilahi kila kukicha badala ya kufanya kazi zake za kiufundi.

 

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba Zahera amechoka na vilio vya fedha za kusaini na mishahara kila kukicha ingawa pedeshee mmoja anayeishi Masaki, Dar es Salaam amemuahidi kwamba wanapambana kuweka mambo sawa.

 

Kocha amewaambia viongozi ni lazima wawalipe wachezaji wote ambao wanadai fedha zao za usajili na mishahara hata nusu kwa sababu wanaitumikia timu na wanaipambania kwa kila hali.

 

Amesema kwamba ni lazima wawalipe wachezaji hao kwani kama siyo hivyo yeye hatarudi kuendelea na Yanga kwa sababu amechoka kuwa msuluhishi wa matatizo ya wachezaji,” kilisema chanzo cha kuaminika ndani ya uongozi wa Yanga.

Uchunguzi wa Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili umebaini kwamba, nusu ya kikosi cha Yanga wanadai fedha zao wa usajili lakini kikosi kizima kinadai malimbikizo ya mishahara isiyopungua mitatu.

STORI NA MUSA MATEJA NA SAIDI ALLY | SPOTI XTRA

Comments are closed.