WEMA APEWA MASHARTI 5 MAZITO, BAADA YA KUANZA BIASHARA

 

Staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu

WEMA si yule! Baada ya kuanzisha biashara yake ya duka la nguo za watoto liitwalo Little Sweetheart, staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu amepewa masharti matano (5) mazito, Risasi limedokezwa. Duka hilo la Wema lililopo Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar, ni la pili baada ya lile la kwanza lililomshinda lililokuwa likiuza lipstick zake za Kiss by Wema lililokuwa maeneo ya Mwenge, Dar.

 

FAMILIA YAINGILIA KATI Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na Wema, baada ya kufungua duka hilo lenye mzigo mkubwa aliofuata mwenyewe nchini China, miezi miwili iliyopita, familia yake iliingilia kati na kumwekea masharti mazito ili lisije likamshinda kama lile la awali.

 

SHARTI LA KWANZA “

Miongoni mwa masharti aliyowekewa Wema na familia yake ni kuwa chini ya dada yake aitwaye Nuru Sepetu. Nuru ndiye meneja wa Wema kwa sasa hivyo ili kumfikia staa huyo lazima upite kwake. “Nuru ndiye anayesimamia kila kitu dukani hapo kuliko kumwachia Wema mwenyewe ambaye wanamjua ana mambo mengi hivyo usimamizi unaweza kumshinda na hata huyo Wema mwenyewe lazima afuate maelekezo ya Nuru.

SHARTI LA PILI

 

“Pili, Wema anatakiwa kujilinda na skendo kwani kadiri atakavyokuwa akichafuka ndivyo atakavyokuwa akiharibu image (taswira) ya biashara kwa maana ya jina la duka. “Aliambiwa kama akileta mambo yake ya skendo za kila kukicha, basi atapoteza hata wateja hivyo lazima ajilinde mno na alinde jina lake kubwa ambalo amekuwa akishindwa kulitumia kwa muda mrefu kumwingizia mkwanja. “Ameelezwa kuwa kama angesimamia vizuri jina lake ni kubwa mno hivyo angekuwa mbali sana kimaisha, siyo kwa kumiliki duka tu bali miradi mikubwa na hata viwanda vikubwa hapa nchini.

 

SHARTI LA TATU

“Tatu, amepigwa marufuku kuhojiwa kila kukicha na vyombo vya habari ambavyo vingine vimelenga kumharibia badala ya kumjenga. “Sasa hivi hatakiwi kabisa kuzungumza na waandishi wa habari, badala yake anayetakiwa kuzungumza kwa niaba yake ni Nuru ambaye ndiye msemaji wake. SHARTI LA NNE “Nne, marafiki wote anatakiwa kutupa kule.

Familia imemwambia kuwa marafiki zake wengi ni wanafiki na wanapenda kumuona tu akiaribikiwa na siyo kumuona akiwa na maendeleo. “Wamemwambia abadilishe aina ya watu wanaomzunguka maana wengi wanakuwa naye wakati wa bata tu, akipata matatizo hawaonekani na ndiyo wanakuwa mstari wa mbele kumsema vibaya na kumcheka.

 

SHARTI LA TANO Tano, Wema anatakiwa kujilinda na anasa za mastaa hasa za kujiachia kwenye kumbi za starehe na kufanya kufuru za kutapanya fedha kwa pombe na mambo mengine. “Ameelezwa kuwa lazima atunze msingi kwa maana ya mtaji, la sivyo utayeyuka na hatakuwa na fedha za kwenda China au kwingine nje ya nchi kuchukua mzigo,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.

 

RISASI MZIGONI Baada ya kupewa masharti hayo, Gazeti la Risasi Jumamosi liliingia mzigoni na kuzama dukani hapo ili kupata
mbivu na mbichi.

 

NURU ACHARUKA Baada ya kuingia dukani hapo na kuomba kuzungumza na Wema, Nuru alimhoji mwandishi alichotaka. Alipoelezwa kuwa mwandishi wetu alitaka mahojiano na Wema alicharuka kwa maelezo kwamba staa huyo haruhusiwi kufanyiwa mahojiano. Nuru alikataa katakata Wema kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote huku akiomba apumzishwe kwa sasa kwenye midomo na macho ya watu ili apate muda mzuri wa kufanya biashara zake.

 

Nuru ambaye hakutaka kujibu hoja moja baada ya nyingine kama alivyoulizwa juu ya masharti hayo matano, alisema ni wakati wa watu kumuacha Wema kufanya mambo ya muhimu ikiwemo kusimamia duka lake hivyo wampe muda afanye biashara na siyo kumfuatafuata kwa mambo yaliyopita kwa manufaa yao binafsi hivyo kwa sasa atasimama kama meneja wake kwa muda.

 

MSIKIE NURU “Jamani naomba Wema apumzishwe tafadhali ili aweze kufanya mambo mengine ya muhimu, imetosha sasa na mimi nitasimama kama meneja wake kwa muda, kwani hakuna watu wengine wa kuwafuatilia zaidi ya Wema? “Nawaomba watu wamwache Wema apumzike na kufanya mambo ya msingi kwa sababu amechekwa vya kutosha,” alimaliza Nuru na kuomba mazungumzo yaishie hapo.
STORI

Loading...

Toa comment