Bocco: Tutawazima Waarabu, Tulieni

Kikosi cha timu ya Simba.

NAHODHA wa Simba, John Bocco, ameweka wazi licha ya kupangwa na timu mbili kutoka mataifa ya Uarabuni katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wamejipanga kuweka rekodi kuhakikisha wanawafunga kila watakapokutana nao na kusonga mbele katika hatua hiyo.

 

Bocco ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliosaidia kikosi hicho kutinga hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika ambapo wamepangwa katika Kundi D. Kundi hilo lina timu za Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria pamoja na AS Vita ya DR Congo huku mechi yao ya kwanza ya hatua hiyo wakitarajia kucheza Januari 11 mwakani.

Bocco ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wameona kundi ambalo wamepangwa na tayari wameanza kujiandaa kikamilifu kuhakikisha wanazifunga timu zote ambazo watacheza nazo katika Uwanja wa Taifa zikiwemo Al Ahly na JS Saoura.

 

“Mashindano haya ni magumu na kundi tayari tumeliona, kwetu hili ni kundi zuri na tutapambana kwa ajili ya kusonga mbele katika kundi kwa kushika nafasi za juu. “Watu wamekuwa wakiona tukipoteza mara nyingi mbele ya timu za Kiarabu lakini kwa msimu huu niwaambie kwamba tutaweka historia kwa kuwachapa wote ambao tutacheza nao.

 

“Sisi hatuchezi kwa historia eti kwamba tulipoteza mechi na timu fulani bali tunacheza kwa kilichopo mbele yetu, kwa hiyo naamini tutajipanga vizuri kwa msimu huu na lengo letu ni kuweka rekodi,” alisema Bocco.

STORI NA SAID ALLY

Loading...

Toa comment