Zahera Ampatia Mbinu Ajibu Kuitwa Stars

Mshambuliaji Ibrahim Ajibu (kushoto) akifanya yake Uwanjani.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amedai kumpatia mbinu kabambe, kiungo wake mshambuliaji Ibrahim Ajibu ili aweze kuitwa na kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike kwa ajili ya kuitumikia katika michezo yake ijayo.

 

Zahera amechukua uamuzi huo baada ya kuona uwezo wa Ajibu unatosha kuisaidia Taifa Stars kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu lakini alikuwa anashindwa kuitwa kwenye kikosi hicho ambacho kitaumana na timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Machi.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema kutokana na uwezo mkubwa alionao Ajibu, amempatia mbinu za kumwezesha kuitwa kwenye kikosi hicho mara moja endapo atahakikisha anamthibitishia Amunike anapokuwa uwanjani kwa kuwa karibu na kila tukio la mpira linapotokea jambo ambalo kwa namna moja anamuona kuelekea.

 

“Mimi naamini katika uwezo mkubwa alionao Ajibu, sema alikuwa na upungufu mchache na nimemwambia aufanyie kazi mara moja na kwa haraka. “Tayari ameshaanza kuyaonyesha, hivyo kwa mwenendo ninaomuona napata imani kubwa kuwa hadi kocha wa Stars atakapofikia kuwaita majina basi atakuwa ameshamhamasisha na hatamuacha.

“Kocha yeyote akija hapa nchini akaona uchezaji wa Ajibu hawezi kubishana na mimi kuwa Ajibu ana kipaji ila alikuwa na upungufu mdogo tu ambao kama mwenyewe akibadilika lazima atacheza kila kikosi cha taifa. “Nimemwambia yeye na wenzake kuwa wahakikishe wanashinda kila mechi yetu ya ligi kwani hadi mwisho tukiwa kileleni hataweza kuita watu nje ya Yanga akaacha wanaoongoza ligi,” alisema Zahera.

STORI NA MUSA MATEJA

Toa comment