SERENGETI LITE WAMEIBUA MENGI SOKA LA WANAWAKE
KINACHOONEKANA kwenye Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu maarufu kama ‘Serengeti Lite Womens Premier League’ kinafurahisha. Kuna mambo mengi ambayo wadau hawakutarajia lakini yanatokea.
Kwanza ushindani umekuwa mkubwa viwanjani, ligi imekuwa na mvuto, mastaa wengi wapya wameibuliwa na vilevile mashabiki wengi wanajitokeza viwanjani haswa Dar es Salaam.
Udhamini wa Serengeti Lite kwenye ligi hiyo kumechangia kuongeza mvuto kwani timu zimewezeshwa zikafanya mambo ambayo mashabiki walikua wakiyatamani.
Ligi hiyo imekuwa na mvuto kiasi kwamba hata baadhi ya timu zimesajili mastaa kutoka nje ya nchi ili kufanya vizuri zaidi.
Ligi hii inaundwa na timu 12 kutoka maeneo tofauti. JKT Queens na Mlandizi Queens zinatokea Pwani, Simba Queens, Yanga Princess na EverGreen Queens zinatokea Dar.
Sisterz FC ya Kigoma, Panama FC (Iringa), Alliance Girls na Marsh Academy za Mwanza, Tanzanite SC (Arusha), Baobab Queens (Dodoma) na Mapinduzi Queens kutoka Njombe.
Kila mkoa hamasa imekuwa ni kubwa zaidi ya msimu uliopita jambo ambalo linaonyesha uwepo wa mdhamini umechangia. Maafande wa JKT Queens ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakitwaa ubingwa huo msimu uliopita pasipo kupoteza mchezo wowote.
Nyota wao ni Fatuma Mustapha. Aliibuka mfungaji bora msimu uliopita baada ya kutumbukia kambani mabao 18. Msimu huu pia ameanza na moto na ana mabao 17 kwenye michezo sita pekee mpaka sasa.
Kabla ya mechi za jana jioni, timu zote zilicheza mara sita huku JKT Queens ikiwa kileleni baada ya kuvuna alama 18 kutokana na kushinda michezo yote sita.
Lakini macho na masikio ya wapenzi wengi wa soka yapo kwa timu mbili ambazo ni watani wa jadi, Simba Queens na Yanga Princess.
Januari 13, mwaka huu zilicheza jijini Dar na Yanga akajikuta akiambulia kipigo cha mabao 7-0 licha ya kuonyesha ushindani.
Nikiwa shuhuda wa mchezo ule, niliona Simba walistahili kushinda kwa zaidi ya mabao hayo kwa sababu uimara wa kikosi chao ambacho inaonekana uongozi umeamua kuwekeza.
Safu ya ushambuliaji ya Simba Queens ikiongozwa na Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ ni imara na imekuwa ikichachafya kwenye ligi hiyo.
Kwenye mechi ya watani wa jadi, fowadi ya Simba ilitengeneza nafasi nyingi ambazo huenda zingezaa mabao mengi zaidi lakini na suala la kukosa uzoefu nalo likachangia.
Gaucho aliifungia timu yake mabao manne huku akikosa nafasi zingine nne ambazo kama angekuwa mtulivu zaidi basi angeweza kuweka mpira kimiani katika nafasi zote alizopata zaidi ya saba.
Yanga licha ya kwamba imeonyesha uhai lakini bado inahitaji kuwekeza kwenye soka la wanawake. W a m e k o s a wachezaji ambao wana uwezo binafsi wa kupambana na kutafuta matokeo ya ushindi na inaonekana hawakufanya maandalizi mazuri.
Simba Queens wanaonekana kuimarika zaidi kadiri siku zinavyozidi kwenda tofauti na Yanga Princess ambayo ni dhahiri inaonekana inakumbana na changamoto kadhaa za nje ya uwanja.
Simba imewaleta nyota wa kimataifa kutoka Burundi, Johelle Bukuru na Asha Djafar ambao wameonyesha kiwango kizuri kinachowapa changamoto wachezaji wazawa.
Kwa hali ilivyo hivi sasa kama Simba wataendelea kukua kwa kasi yao hii inayoonekana basi bila shaka msimu ujao wanaweza kutwaa taji hili.
Yanga wanahitaji umakini zaidi kwenye usajili ili kufika pale walipo wenzao kwa sababu timu yao inahitaji maboresho machache ili iwe na uwezo wa kupambana kwenye kiwango cha juu zaidi katika mashindano hayo na mengine.
Comments are closed.