The House of Favourite Newspapers

Man United Yaipiga Arsenal 3-1, Yaitupa Nje FA Cup

ARSENAL ikiwa kwenye Dimba la Emirates usiku wa kuamkia leo, imekubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Manchester United kwenye mchezo wa Kombe la FA raundi ya nne. Hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Kocha wa United, Ole Gunnar Solskjær, anakutana na Kocha wa Arsenal Unai Emery, tangu waanze kuzinoa timu zao.

Katika mchezo huo ambao umemaliza safari ya Arsenal ya kutwaa ubingwa wa FA mara ya 14 baada ya awali kuutwaa mara 13, United walionekana kuanza taratibu lakini kwa umakini wa hali ya juu.

Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Alexis Sanchez ambaye alipoondoka hapo Januari, mwaka jana, ndiye alikuwa wa kwanza kuifungia United bao safi katika dakika ya 31 akipata pasi kutoka kwa Romelu Lukaku.

Iliwachukua United dakika mbili tu kupata bao la pili ambapo Jesse Lingard alitumia uzembe wa mabeki wa Arsenal na kuifungia timu yake akipata pasi kutoka kwa Lukaku. Baada ya kufungwa mabao hayo, Arsenal ambao walipoteza nafasi nyingi waliamka na kuendelea kupambana ambapo walijipatia bao moja kupitia kwa Pierre Aubameyang
ambaye alimalizia pasi safi ya Aaron Ramsey katika dakika ya 43.

Arsenal waliendelea kutawala kipindi cha pili, lakini dakika ya 83 Paul Pogba aliambaa na mpira na kupiga shuti kali lilopanguliwa na Petr Cech na kumkuta, Anthony Martial, akapachika bao la tatu na kuhitimisha ushindi huo wa mabao 3-1. Sasa ina maana United wameendelea kutopoteza mchezo tangu walipoanza kunolewa na Solskjær.

Comments are closed.