The House of Favourite Newspapers

T-Pesa kuanzisha mfumo wa malipo kwa kutumia card

Mkuu wa Huduma za T- PESA, Moses Alponce (wa pili kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Kampuni ya PayLink ya Korea, MoonKyu Lee (wa pili kushoto)  wakisaini leo jijini Dar es Salaam makubaliano ya mradi wa kutengeneza mfumo wa malipo kwa kutumia kadi (T Card). 
Wakibadilishana nakala za makubaliano yao mara baada ya kusaini leo jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia kulia na kushoto ni wanasheria wa pande zote.
Wakionesha nakala za makubaliano ya mradi wa kutengeneza mfumo wa malipo kwa kutumia kadi (T Card) utakaotumika kulipia huduma mbalimbali nchini Tanzania. 
Picha ya pamoja ya viongozi waandamizi wa kampuni zote mara baada ya hafla ya kusaini mkataba huo wa ushirikiano kibiashara.

 

 

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation, kupitia mtandao wake wa huduma za kifedha wa T-PESA pamoja na wadau wa kibiashara, Kampuni tatu kutoka nchini Korea zimesaini mradi wa kutengeneza mfumo wa malipo kwa kutumia kadi (T Card).

 

 

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Makao Makuu ya TTCL leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Huduma za T- PESA Ndugu Moses Alponce, alisema mfumo huo unaotumia teknolojia za kisasa ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kuonesha mahitaji makubwa ya huduma za malipo yasiyotumia fedha tasilimu.

 

 

Aidha aliongeza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutarahisisha shughuli za kibiashara na kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika kukusanya kikamilifu kodi za Serikali kutoka kila miamala itakayofanyika, sambamba na kuongeza ufanisi katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

 

 

Mfumo huo unaotekelezwa na T-Pesa kwa kushirikiana na wadau wake kibiashara kutoka Jamhuri ya watu wa Korea katika muunganiko wa Kampuni tatu, ambazo ni PayLink Korea, KEH Hana Card pamoja na ATECT & Company unakuwa wa kwanza kuletwa na huduma za fedha kwa kutumia simu za mikononi nchini Tanzania.

 

 

“Kampuni hizi zitashirikiana na T PESA katika zoezi la kuandaa, kupanga na kutengeneza Mfumo wa kadi za NFC na POS Cashless Ecosystem,” alisema Alponce.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya PayLink ya Korea, MoonKyu Lee akiwakilisha kampuni hizo alisema kuingia kwa ushirikiano katika mfumo huo utaongeza uwazi katika miamala ya kifedha jambo ambalo litaongeza mapato ya kodi kwenye mifumo ya malipo nchini na kuleta maendeleo.

 

 

Ikiwa sasa ni takribani miaka miwili tangu kuanzishwa kwake, T PESA imekuwa na mchango mkubwa katika huduma za Fedha mtandao Nchini, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya TCRA toleo la mwaka 2019, T PESA ni moja ya huduma zinazokua kwa kasi kubwa ikiwa na Mawakala 10,000, wateja laki 320,000 wanaozungusha miamala ya takribani Tsh Bilioni 4.

Comments are closed.