The House of Favourite Newspapers

Jinamizi hili la ratiba linaua soka la Tanzania

Kikosi cha timu ya Azam FC.

 

TUNAPOIZUNGUMZIA Ligi Kuu Bara, basi tunaizungumzia ligi ya levo za juu kabisa katika soka la Tanzania Bara na bingwa ndiye anaiwakilisha nchi kwenye mi­chuano ya Ligi ya Mabingwa Af­rika.

 

Hakuna asiyefahamu ukubwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa Afrika michuano hiyo ndiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu.

 

Sasa inapotokea kwenye Ligi Kuu Bara kuna vitu haviendi sawa, lazima tuzungumze ili wahusika kama ni waelewa, basi wataya­fanyia kazi hayo mapungufu yal­iyopo.

Kwa misimu mingi, jambo hili la timu kuwa na viporo vingi lime­zungumzwa, lakini kwa msimu huu limezungumzwa zaidi kuto­kana kuonekana kwamba wa­husika kama vile hawaelewi watu wanazungumza nini.

 

Tazama hivi sasa msimamo wa Ligi Kuu, vinara Yanga na wa­naofuatia, Azam FC, wote wa­mecheza mechi 25, bado mechi 13 wamalize msimu, lakini Sim­ba wanaoshika nafasi ya tatu, wenyewe wamecheza mechi 19, wana mechi 19 ili wamalize msimu.

 

Achana na hao. Kuna timu kama Lipuli, Ruvu Shooting, Alliance, Stand United na Mwadui, zina mechi 10 tu mkononi ili kumali­za msimu. Hapo hakuna usawa hata kidogo.

 

Ili kuondoa dhana hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) mna­paswa kukaa chini na kuhakiki­sha msimu ujao hili halijitokezi tena.

 

Msimu huu tukubali kwamba mmeshindwa kulisimamia hilo kwa sababu misimu yote inafa­hamika wazi kwamba huwa kuna mashindano mbalimbali tena mengi yapo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

 

Msimu ujao hatutaki hili lijirudie, kabla ya kupanga ratiba yenu ya msimu, itazameni kwa kina Kalenda ya Caf na Fifa. Hapo mtakuwa mmetibu huu ugonjwa, vinginevyo hakutakuwa na jipya.

STORI na Bodi ya Uhariri/Maoni | CHAMPIONI IJUMAA

Comments are closed.