The House of Favourite Newspapers

MAN UTD YATINGA ROBO KIBABE, YAIPIGA PSG 3-1 PARIS

MAWAIDHA mazito ya kocha wa zamani, Alex Ferguson yalikuwa chachu ya Manchester United kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuiliza Paris St. Germain mabao 3-1 kwenye mechi ya marudiano ya mtoano wa 16 bora iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Parc de Princes jijini Paris.

 

Manchester United `ilipindua matokeo’ ugenini baada ya mchezo wa kwanza kulala mabao 2-0 nyumbani kwenye Uwanja wa Old Trafford, Februari 12, mwaka huu na kufanya sasa kusonga mbele kwa sheria ya goli la ugenini baada ya timu hizo kufungana 3-3.

Ushindi huo wa mabao matatu umeifanya Manchester United kuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao ya ugenini. Manchester United imeibuka kidedea baada ya kupata busara za kocha wao wa zamani, Ferguson, ambaye alisafiri pamoja na wachezaji wa timu hiyo kwenda Ufaransa juzi.

Kocha wa Mancheter United, Ole Gunnar Solskajer alitaka kuchota ujuzi wa Ferguson kwani enzi hizo akiinoa timu hiyo alikuwa anasifika kwa `kupindua matokeo’ ikitokea timu yake imefungwa nyumbani na kutakiwa kusaka matokeo mazuri ugenini. Mashabiki walio wengi wa soka wanakumbuka wakati Ferguson alipoiongoza Manchester United kuitoa Juventus kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.

Manchester United ililala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Old Trafford lakini ikaenda ugenini nchini Italia na kushinda mabao 3-2. Katika mchezo wa jana, mabao mawili ya Manchester United yalipachikwa na straika wa timu hiyo, Lukaku ambaye ameweka rekodi ya kupachika mabao mawili katika mechi tatu mfululizo. Alipachika idadi hiyo ya mabao kwenye mechi za Ligi Kuu England dhidi ya Crystal Palace na Southampton hivi karibuni.

Manchester United ilianza mchezo wa jana kwa kupata bao la kwanza mapema dakika ya pili tu kufuatia makosa ya beki wa PSG, Thilo Kehrer kutoa pasi mbovu kwa kipa wake, Gianluigi Buffon lakini Lukaku aliuwahi mpira na kumlamba chenga kipa na kuujaza mpira wavuni.

 

PSG ilisawazisha mnamo dakika ya 12 baada ya straika wake Kylian Mbappe kuchukua mpira kwenye eneo la Manchester United na kutoa pasi kwa Juan Bernat, ambaye aliunganisha mpira wavuni kiulaini, Manchester United iliongeza bao la pili katika dakika ya 30 kufuatia makosa ya kipa Buffon kutema shuti la Marcus Rashford na Lukaku alikuwa karibu na akaujaza mpira wavuni.

 

Rashford ndio alipachika bao lililoipeleka Manchester United robo fainali baada ya kufunga kwa penalti katika dakika ya 92 kufuatia beki wa PSG, Presnel Kimpembe kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Hadi tunakwenda mitamboni mechi nyingine kati ya Porto na Roma iliongezewa dakika 30 kutokana na timu hizo kuwa zimefungana jumla ya mabao 3-3.

Comments are closed.