The House of Favourite Newspapers

MAFUNZO YA NDOA PADRI AWATAJA WEMA, MONDI KANISANI

 

MOROGORO: KATIKATI ya mafunzo ya ndoa, Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kigurunyembe Jimbo la Morogoro, FR Respicius Nyamwilu almaarufu FR Res amewataja mastaa wawili wakubwa Bongo, Wema Isaac Sepetu wa Bongo Movies na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutoka Bongo Flevani.

 

Tukio hilo lilijiri kwenye parokia hiyo ya Kigurunyembe ambapo padri huyo aliwataja mastaa hao alipokuwa akikemea uchumba sugu akidai jambo hilo halimpendezi Mwenyezi Mungu.

 

Wema na Diamond au Mondi waliwahi kuwa ‘wachumba sugu’ kabla ya kutengana na kila mmoja kuchukua hamsini zake. Ibada hiyo pia ilikuwa ya kumuombea aliyekuwa mwandishi wa habari, marehemu Lilian Justice Chuwa aliyefariki dunia hivi karibuni.

 

MSIKIE PADRI

“Siku hizi kumekuwa na uchumba sugu, watu wanakaa kwenye uchumba kwa muda mrefu bila kufunga ndoa wakichunguzana kwa miaka mingi hadi wanazaa watoto bado tu wanachunguzana. “Hivi pikipiki au gari vina thamani kuliko binadamu?

 

“Unaweza kwenda dukani au show room ya magari, ukamwambia mwenye show room, hebu nipe hili gari au pikipiki nikaichunguze kwa muda, ikinipendeza nakuja kuilipia, nani atakubali jambo hilo?

 

“Ukalichakaze gari lake jipya zaidi ya miezi sita kisha ulirudishe dukani useme hukulipenda hivyo unakwenda kununua gari duka lingine, ni muuza gani atakubali jambo hilo?

 

“Sasa kwa nini wewe binadamu mwenye thamani kubwa kuliko hayo machuma unakubali kuingia kwenye uhusiano na mtu, anakuchunguza miaka nenda, miaka rudi hadi mnazaa watoto kisha anakuambia hakutaki anakwenda kuoa au kuolewa na mwingine wakati ameshakupoteza muda?

THAMANI INAPUNGUA

“Na kama ni mwanamke, tayari umeshazalishwa na thamani yako imepungua. “Niwaombeni, wenye nia ya kweli ya kuingia kwenye ndoa msichukue muda mrefu kuchunguzana. “Niwaambieni jambo jambo moja, wakati huyo mpenzi wako anakuchunguza, ujue hauko peke yako, mko wengi mnaochunguzwa! ”Hakuna binadamu aliyekamilia. Kama mmependana mnafunga ndoa kisha mmoja anavumilia matatizo ya mwenzi wake huku maisha yanaendelea

 

WEMA NA DIAMOND

“Kuna baadhi ya watu wakati viongozi wa dini wakitoa mahubiri kanisani au mawaidha msikitini, wao huwa wanauchapa usingizi ndani ya nyumba za ibada. “Hivi karibu kulikuwa na mechi kubwa pale Dar, timu f’lani ya Taifa ilikuwa ikicheza na timu nyingine, uwanja ulijaa kwelikweli, kwa dakika zote 90 hakuna aliyesinzia pale uwanjani. “Na baada ya timu hiyo mwenyeji kuibuka na ushindi, kuna kiongozi mmoja alitoa ofa ya vinjwaji.

 

“Pia kwenye vinywaji hakuna aliyesinzia, walikesha usiku kucha kushangilia ushindi huo. “Mtu mwingine ukiwa nyumbani kwenye runinga unaangalia Muvi za Wema Sepetu (kama Madam, A Point of No Return, Day After Death, Heaven Thanks, More Than Woman na nyinginezo) au Nyimbo za Diamond (kama Number One, Mawazo, Mdogomdogo, African Beauty, Nana, Baila na nyinginezo) mbona husinzii? “Kwa nini kiongozi wa dini akihubiri, tena kwa dakika chache, siyo dakika 90 wala 100 baadhi yao wanasinzia?” Alihoji FR Res.

 

Baada ya madongo hayo, baadhi ya watu waliokuwa wakisinzia kwenye ibada hiyo walizinduka na kupepesa macho huku wakijikausha.

 

PONGEZI

Baadhi ya watu waliohudhuria ibada hiyo walimpongeza padri huyo wakisema mahubiri yake yalijaa mafundisho ya kweli dani yake.

“Kweli siyo jambo zuri, unamchumbia mtoto wa mtu, unakaa naye kwa muda mrefu hadi unamzalisha watoto wawili hadi watatu kisha unamuacha, unakwenda kuoa mwanamke mwingine,” alisema Joyce Joseph, mmoja wa wahudhuriaji wa ibada hiyo.

 

Naye Agostino Pius alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya mahubiri hayo alisema; “Hilo si kwa wanaume tu, hata wanawake, unaweza kumuoa kwa ndoa, akipata mwanaume mwenye pesa anavunja ndoa, anakwenda kuwekwa kinyumba na mwanaume mwingine.

 

“Jambo hilo ni chukizo kubwa mbele za Mungu kwani ndoa ni jambo la kheri, mtu akivunja ndoa, Mungu anachukia sana.

“Kwa mantiki hiyo, huyo mtu hawezi kuwa salama katika maisha yake, ataandamwa na mikosi kila kukicha.”

 

UCHUMBA SUGU

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo, uchumba sugu ni kuanzia miezi sita na kuendelea. Wema na Diamond walidumu kwenye uhusiano kwa zaidi ya miaka miwili hivyo ni dhahiri walikuwa miongoni wa kundi la wachumba sugu hivyo huenda mahubiri ya padri huyo yaliwagusa pia mastaa hao.

Stori: Dunstan Shekidele, Amani

KAYUMBA – “UWOYA Mzuri, WANAMTONGOZA Sana, Hajawahi Kuninunia”

Comments are closed.