Serengeti Boys yawachefua Watanzania

Serengeti Boys.

TUKILIA haisaidii. Wala tukicheka haisaidii. Ni janga na fedheha ya kitaifa. Hakuna namna, lazima tuinamishe vichwa chini tutoke kimyakimya. Maneno machache tu ya kizalendo kwa Serengeti Boys.

 

“Asanteni kwa kushiriki na kwaherini vijana wetu.” Tanzania imekosa kila kitu. Hakuna cha tiketi ya Kombe la Dunia wala ubingwa wa Afcon U-17.

Serengeti Boys wakiwa wenyeji wa michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya Afrika, jana jioni waliaga rasmi mashindano hayo kwa aibu huku wakizomewa na baadhi ya mashabiki.

Timu hiyo ilipigwa mabao 4-2 na Angola jana katika mechi ambayo Watanzania walitegemea angalau ushindi kwa Serengeti ili wavuke kwa hesabu za mezani, lakini mambo yakagoma wakaambulia aibu.

 

Katika mechi ya jana, mabao ya Serengeti yalifungwa na Omary Jumanne na Agiri Ngoda huku yale ya Angola yakifungwa na Telson Tome, Osvaldo Kapemba(mawili) na David Nzanza Watanzania walipiga pasi 282 ndani ya dakika 90 dhidi ya 275 za wageni lakini haikusaidia, umiliki wa mpira ilikuwa ni asilimia 52 kwa Serengeti dhidi ya 48.

Lakini pia umakini wa pasi Angola walikuwa asilimia 65 dhidi ya 64 za Serengeti na faulo na kona zilikuwa za kumwaga.

 

Serengeti imefungwa mechi zote tatu dhidi Nigeria 5-4, Uganda 3-0 na ile ya jana, hivyo kumaliza kundi wakiwa hawana pointi yoyote.

Kabla ya mashindano hayo Serengeti ilikuwa imebeba ubingwa wa Cecafa na Cosafa. Makocha mbalimbali juzi walikuwa wakilalamikia umri wa wachezaji wa timu shiriki kwenye michuano hiyo huku Serengeti, Morocco, Senegal na Angola zikitajwa kama timu pekee zenye umri sahihi wa mashindano.

PICHA NA MUSA MATEJA, HABARI NA SAID ALLY -GPL


Loading...

Toa comment