visa

Taifa Stars iandaliwe kucheza usiku Misri

PRESHA ya Wachezaji wa Tanzania ni kucheza usiku. Wengi hawajazoea kucheza mida hiyo kutokana na ukweli kwamba tangu wanapokuwa wadogo wamezoea mechi zinachezwa mchana au jioni.

 

Hata miundombinu ya Tanzania si rafiki kucheza usiku kwani ni viwanja vitatu tu nchi nzima ambavyo vinaweza kuchezewa usiku, ule wa Azam, Taifa na JK Park. Vyote vya Dar es Salaam.

 

Mara kadhaa timu zetu zinapopangiwa kucheza na timu za Arabuni hususani Misri hukumbana na changamoto kubwa kwani klabu nyingi za huko zimezoea kucheza usiku ambayo ni mazingira ya baridi. Hivyo mara kadhaa timu za Tanzania zimekuwa zikipoteza na kusingizia baridi hilo. Maoni yetu ni kwamba Taifa Stars iandaliwe kisaikolojia kwa kucheza usiku.

 

Mechi zao zote tatu kwenye hatua ya makundi zinachezwa kuanzia majira ya saa 2 usiku na kuendelea hivyo ni vyema wakianza kuizoea hali hiyo ili tusipate aibu kwenye fainali hizo kwani hakuna namna lazima tucheze usiku. Wenzetu tuliopo nao kundi moja Algeria na Senegal wamezoea hali hiyo, Kenya ina wachezaji wengi wanaocheza nje nao hali hiyo siyo tatizo kwao.

 

Ishu ni kwetu Taifa Stars inayoundwa na asilimia tisini ya wachezaji waliozowea kucheza kwenye jua kali na mwanga wa mchana. Fainali hizo zinaanza Juni 21 hadi Julai 19.

 

Tunapaswa kujianda kwa dhati kuanzia viongozi mpaka wachezaji na benchi la ufundi. Katika mashindano, kitu kikubwa kinachoiwezesha timu kufanya vizuri ni maandalizi ambayo yanatakiwa kufanywa mapema, hivyo basi kwa muda huo ambao watapata TFF inatakiwa kusimamia timu kuona inatumia muda huo kwa kufanya maandalizi ya nguvu na si vinginevyo.

 

Kama tunataka kufanya vizuri, inabidi mikakati iandaliwe mapema kwa muda ambao umesalia kama hivi ambavyo wametoa taarifa kuwa Stars itajipima na Misri kitu ambacho ni kizuri.

 

TFF wasiishie hapo kwa Misri wanatakiwa kupata michezo mingine ya maana ya kirafiki ambayo itakuwa msaada kwa kikosi chetu kiwe fiti isi tusiwe wasindikizaji. Wachezaji nao licha ya maandalizi hayo wanatakiwa kuweka akili zao uwanjani wakijua kwamba wanakwenda vitani, zile si mechi za kirafiki ni fainali za Afrika.

 

Pia wachezaji na benchi la ufundi wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia` kutokana na hali ya hewa ya baridi nyakati za usiku ambazo Stars itakuwa ikicheza. Tunaaamini kabisa wachezaji wataweka bidii kuepuka yale yaliyowakuta Serengeti Boys ambao walishindwa kutamba kabisa kwenye michuano ya Afcon kwa vijana ambayo leo itafika tamati hapa jijini Dar es Salaam.

 

Kocha wa Stars, Emmanuel Amunike anatakiwa kutambua ana kazi kubwa na afahamu Watanzania wanamuangalia yeye hivyo katika maamuzi yake ya kuandaa kikosi inabidi achague wachezaji ambao watakuwa msaada na imara kuweza kuibeba nchi kwenye michuano hiyo.

 

Lakini pia, Amunike aanze sasa kuwachunguza wapinzani wake mmoja baada ya mwingine ili ajue ataenda na mbinu gani katika michuano hiyo. Sababu tunafahamu kuwa kundi ambao amepangwa sio kundi rahisi hata kidogo kwanza wao wameshiriki michuano hiyo mara nyingi zaidi na wengine hata kutwaa ubingwa wa Afrika.

 

Hivyo ni vyema Amunike na wachezaji wake wakapambane kwa bidii na kufahamu kuwa wanatengeneza heshima ya nchini si vinginevyo. Tunawatakiwa maandalizi mema.
Toa comment