Majaliwa Ajiandikisha Wilayani Ruangwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amejiandikisha kwenye kituo cha shule ya msingi Nandagala, wilayani Ruangwa, Lindi ili aweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

 

Majaliwa ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa amejiandikisha kijijini kwao leo asubuhi (Jumamosi, Oktoba 12, 2019) akiwa na mkewe  Mary Majaliwa.

 

Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, amesema zoezi la kujiandikisha ni la kitaifa na ni haki ya kila Mtanzania ili aweze kuchagua kiongozi amtakaye au aweze kugombea kwenye uchaguzi utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu.

“Kila mmoja anapaswa kuja kujiandikisha. Zoezi hili ni tofauti na lile la uchaguzi mkuu,” alisema.

Kuna watu wanafanya upotoshaji wa makusudi, wanawadanganya wenzetu kwamba kama huna kadi ya uchaguzi huna haja ya kujiandikisha. Hii siyo kweli, hiyo kadi ni ya uchaguzi wa mwakani,” amesema.

 

Mara baada ya kujiandikisha, Majaliwa alipita katika vijiji vya Chimbila B, Chimbila A, Michenga (Jerusalem), Michenga (Misri), Nangumbu na Nanganga.

Waziri Mkuu alizungumza na wanavijiji waliosimama njiani ambao waliwahimiza wajiandikishe kwa ajili ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.

 


Loading...

Toa comment