The House of Favourite Newspapers

Mzee Akilimali: Yanga SC Wanapigwa na Pyramids

KATIBU wa Baraza la Wazee wa Yanga, mzee Ibrahim Akilimali ameibuka na kusema kuwa haoni dalili za Yanga ikiitoa Pyramids ya Misri katika mchezo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na uongozi wa timu hiyo kugoma kuwapa timu wazee kuishughulikia.

 

Mzee Akilimali ametoa kauli hiyo kufuatia Yanga kupangwa na timu hiyo katika hatua ya mtoano ambapo inatarajia kucheza mchezo wa kwanza Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kabla ya kuelekea nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, mzee Akilimali alisema kuwa wazee wa timu hiyo wamekuwa wakiiomba kwa ajili ya kuiweka sawa kabla ya kucheza na Waarabu hao wa Misri lakini wamekuwa wakipigwa chenga na uongozi wa timu hiyo bila kuwapa majibu ya maana.

 

“Niwe mkweli kwamba sioni dalili za Yanga ikiwaondoa Waarabu hasa kwa timu ambayo tupo nayo kwa sababu ukiangalia wachezaji wetu wote wamefungwa hawana uwezo wa kushindana kabisa, wanahitaji kufunguliwa lakini uongozi bado unatuwekea ngumu kila tunavyowaambia.

 

“Sisi tunataka watu ili tufanye mambo yetu na tuweze kufuzu makundi lakini wao hawana mpango wowote wa kutupa zaidi ya kutukimbia, wamepeleka mechi Mwanza lakini haiwezi kusaidia chochote maana kama unasajili wachezaji halafu kwao bado wanagombea tuzo kubwa ila hapa wanaonekana weupe, ndiyo wajue kama wamefungwa,” alisema mzee Akilimali.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.