Kocha Mbelgiji Ashusha Straika Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems.

SPOTI Xtra limegundua kwamba Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems tayari ana majina matatu mezani ya wachezaji atakaowasajili kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu.

 

Kocha huyo hivi karibuni alieleza malengo yake ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji mara baada ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kutimkia Klabu ya Ittihad ya jijini Alexandria nchini Misri mwishoni mwa msimu uliopita.

Timu hiyo hivi sasa inamtegemea Mnyarwanda, Meddie Kagere kwenye safu ya ushambuliaji kutokana na mshambuliaji wake John Bocco kusumbuliwa na majeraha ya goti kwa muda mrefu huku akiikosa michezo minne ya Ligi Kuu Bara.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kocha huyo ana majina ya wachezaji watatu kutoka nchi za Afrika Magharibi ambazo ni Ghana, Ivory Coast na Nigeria.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha huyo wakati usajili wa dirisha kubwa haujafungwa kabla ya kuanza kwa msimu huu, alitoa mapendekezo ya kumsajili mshambuliaji mmoja hatari mwenye uwezo zaidi ya Kagere, Bocco na Okwi.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya kumkosa mshambuliaji wa aina hiyo, akamsajili Mbrazili, Wilker Da Silva ambaye hakuwa pendekezo lake la kwanza.

“Kocha tayari ana majina matatu mezani mwake ya washambuliaji kutoka mataifa ya Afrika Magharibi ambao wapo kwenye mipango yake kwa ajili ya kuwasajili katika usajili wa dirisha dogo.

 

“Hiyo ni baada ya Wilker kutokidhi viwango vya aina ya mshambuliaji anayemuhitaji na kikubwa anataka mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao zaidi ya Kagere na Bocco,” kilisema chanzo chetu.

 

Alipotafutwa Aussems kuzungumzia hilo alisema: “Kabla ya usajili wa dirisha kubwa kufunguliwa nilitoa mapendekezo ya kusajiliwa mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga zaidi ya Kagere.

“Lakini uongozi haukunipatia, hivyo nimepanga kuiboresha safu hiyo na lazima nisajili mshambuliaji mwingine hatari zaidi ya Kagere.”

Toa comment