The House of Favourite Newspapers

Afariki kwa Kunywa Pombe Kupita Kiasi

0

MKAZI  wa Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Nkuba Mawe (27),  amekutwa amefariki dunia kwenye vibaraza vya maduka katika Mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga,  eneo ambalo alikuwa akiishi kwa sasa kwa madai ya kunywa pombe kupita kiasi.

 

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana Jumatano Februari 19, 2020,  ambapo wananchi wa eneo hilo walimkuta  amekufa na na kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa huo.

 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Solomoni Najulwa, alisema mara baada ya kupewa taarifa na wananchi alifika eneo la tukio na akatoa taarifa kwa jeshi la polisi ambapo walifika na daktari wa hospitali ya mkoa kufanya uchunguzi na kubaini pombe ndiyo imemuua.

Naye daktari kutoka hospitali ya mkoa huo wa Shinyanga, Richard Mwikambe, akiwa eneo la tukio alisema ni kijana huyo hajauawa kwa kupigwa, bali amefariki dunia kwa sababu ya kunywa pombe kupita kiasi, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kunywa pombe nyingi jambo ambalo ni hatari kiafya.

 

Aidha, mmoja wa ndugu wa marehemu Machiya Nyambo, alisema ndugu yao huyo alikuwa akifanya kazi za ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali ya Shinyanga mjini, na kubainisha tayari wameshawasiliana na ndugu wengine kutoka Ukenyenge ili wafanye taratibu za kuusafirisha mwili na kuuzika.

 

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Deborah Magiligimba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kubainisha hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi la polisi, ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa na ndugu zake watakabidhiwa kwa ajili ya mazishi.

 

Leave A Reply