40 IMETIMIA! ‘ALIYECHEZEA SHARUBU’ SERIKALI YA JPM ANASWA

40 YAKE IMETIMIA! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tukio la Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kumnasa kijana aliyefahamika kwa jina la Lazaro Isack (32) kwa kutuhumiwa kuwatapeli watu kupitia ajira za serikalini. 

 

Kijana huyo mkazi wa Mtaa wa Machinjioni, Kata ya Mhandu katika Wilaya ya Nyamagana amenaswa kufuatia madai kuwa, amekuwa akijifanya ni mtumishi wa serikali na kwa kutumia nyaraka za kughushi amekuwa akiwalaghai watu kuwa atawapatia ajira kwenye taasisi za umma.

 

Mtuhumiwa huyo alikamatwa hivi karibuni huko Mtaa wa Igoma baada ya kuwekewa mtego na polisi na baada ya kupekuliwa alikutwa na nyaraka hizo bandia za serikali.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna wa Msaidizi (ACP) Jumanne Muliro alisema, jeshi hilo limejikita kwenye mfumo wa kudhibiti vitendo vya uhalifu ili kuupunguza na kuwafanya wananchi waishi kwa amani na usalama.

 

Alisema askari wake hawatalala katika mapambano dhidi ya uhalifu wa aina mbalimbali ambapo linamshikilia Lazaro kwa madai ya wizi wa mtandao, kughushi nyaraka za serikali na kuzitumia kuwalaghai watu kuwapatia ajira kwenye taasisi za umma.

 

Mtuhumiwa huyo kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi amewaliza watu wengi wanaotaka ajira serikalini kwa njia ya mkato na kujipatia fedha akitumia nyaraka hizo bandia za serikali ilhali akijua kuwa ni uongo na hana uwezo wa kuwapatia ajira.

 

ACP Muliro alieleza kuwa mtuhumiwa huyo wakati anakamatwa alikutwa akiwa na kitambulisho cha kazi cha VODACOM CAP VIEW Ltd kikiwa na jina lake, kisha polisi walifanya upekuzi kwenye makazi yake na kukuta nyaraka mbalimbali na picha za watu aliokwisha kuwatapeli kuwapa ajira.

“Ajira za serikali hutolewa kwa utaratibu na zinatangazwa ili wenye sifa waombe kwa utaratibu uliowekwa. Sasa huyu alikuwa akijifanya mtumishi wa serikali, amewatapeli watu kwa kisingizio cha kuwapatia ajira.

 

Alipokamatwa na kupekuliwa alikutwa na nakala 34 za utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) za TRA za mikoa mbalimbali, leseni za biashara za duka la rejareja mali ya Charles Itango na ya Shukuru R.Almas,” alisema.

 

Kamanda huyo wa polisi alizitaja TIN hizo 34 na mikoa yake kuwa ni Mwanza 19, Pwani 6, Dar es Salaam 3, Mtwara 2 na nakala moja moja za mikoa ya Dodoma, Geita, Shinyanga na Kagera.

 

Pia alikutwa na karatasi yenye namba za simu mbalimbali na orodha ya majina ya watu aliowalaghai na picha 25 za rangi za ukubwa wa stampu, karatasi ya Log Book ya M-PESA, fomu ya wakala mwakilishi wa M-PESA, flash mbili za ukubwa wa GB 16 na 08 pamoja na morderm ya Airtel.

 

Aidha, alieleza kuwa jeshi hilo linaendelea na mahojiano na mtuhumiwa wa ajira na makosa ya mtandao ili kubaini mtandao wa watu anaoshirikiana nao kufanya uhalifu huo ili sheria ichukue mkondo wake.

MAGUFULI AMWAGA ‘MACHOZI’ AKIAGA MWILI WA MENGI


Loading...

Toa comment