The House of Favourite Newspapers

40 IMETIMIA! ATUMIA FURSA YA AJALI AKIONA CHA MOTO

MOROGORO: 40 yake imetimia! Jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Chande amekamatwa na polisi akidaiwa kutumia fursa kwa kuiba vifaa vya gari baada ya kutokea kwa ajali ya gari kuligonga gari moshi la mizigo, Mtaa wa Kilimahewa mkoani hapa.

 

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa majina ya Shaban Ali alikuwa na haya ya kusema.

 

“Hii ni mara ya pili gari kugonga treni mtaa huu. Miezi miwili iliyopita nyumbani kwa bondia Francis Cheka, teksi ililigonga treni, baada ya ajali ile wafanyakazi wa reli waliweka vizuizi kwa maana ya kuchimba mitaro njia zisizo rasmi zinazokatiza kwenye reli. Leo tena mtaa huu Toyota Canter nayo imeligonga treni,” alisema shuhuda huyo.

 

Alisema kimsingi hiyo sio njia sahihi ya gari kupita, dereva wa gari lililopata ajali alilazimisha kupita njia ya panya ambapo tairi za mbele zilifanikiwa kuvuka mtaro na kutua katikati ya reli huku tairi za nyuma zikikwama kwenye mtaro.

 

Baadaye dereva aliyekuwa na mtu mmoja kwenye gari walishuka na kuanza kulisukuma gari hilo bila mafanikio na wakati wakiendelea na zoezi hilo treni ya mizigo ilifika na kuligonga gari ambapo dereva na abiria wake, walikimbia.

 

“Akatokea jamaa aliyedaiwa mwizi aitwaye Chande anayeuza mchele karibu na sido, alikatiza hapa kwenye ajali na alipoona wenye gari wamekimbia, aliingia ndani ya gari na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo Fire extinguisher (kifaa cha kuzimia moto).

 

“Askari wawili wa reli waliokuwa wakisindikiza treni hii ya mizigo walifika na kumkamata jamaa huyu, huenda amekuwa akifanya vitendo hivyo vya kudokoa kwa muda mrefu lakini leo arobaini yake imetimia,”alidai shuhuda huyo.

 

Mwandishi wetu ambaye pia anamfahamu jamaa huyo alipomuuliza kwa nini ameiba vifaa kwenye gari alijibu. “Shekidele (mwandishi) unanifahamu vizuri, sina tabia ya wizi, nimetoka msikitini naelekea ofisini kwangu nikakuta ajali hii, hii Fire extinguisher imeanguka nikaiokota afande akadai nimeiba,”alisema Chande.

 

Alipoulizwa ajali imetokea na vitu kusambaa, ataokotaje kifaa eneo la ajali? Chande alishindwa kujibu ambapo askari polisi aliyemkamata alimkwida kibindo na kuondoka naye.

 

Mkuu wa Stesheni ya Gari Moshi Morogoro, Salvatory Kimaro alipozungumza na mwandishi wetu alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

 

“Ni kweli ajali hiyo imetokea jana (Ijumaa) jioni Kilimahewa jirani na ofisi za Wakala wa Barabara Mkoa wa Morogoro. “

 

Dereva wa ile gari baada ya kuona gari lake ni bovu aliamua kuwakwepa trafiki kwa kupita njia za panya na matokeo yake ameigonga treni yetu ya mizigo iliyokuwa ikielekea mikoa ya bara kisha yeye kukimbia, tunaendelea kumtafuta, treni imekaguliwa na imeendelea na safari,” alisema mkuu huyo wa stesheni  ya treni.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.