40 YA MTOTO WA KIBA USIPIME!
DAR ES SALAAM: KING atabaki kuwa King tu! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia sherehe kubwa ya kutimiza siku arobaini (40) ambayo staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ amepanga kumuangushia mwanaye wa kiume, Keyaan Ali, Gazeti la Ijumaa lina ‘exclusive’.
Kiba alimposti mwanaye huyo mapema wiki hii katika ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram wenye zaidi ya wafuasi milioni 3.6 ambapo kwa mara ya kwanza, mashabiki wake walimuona na kuanza kumpongeza kwa kuweka maoni yao mbalimbali.
Wengi wao walifanya hivyo kwani hawakumuona mtoto huyo tangu alipozaliwa Februari 27, mwaka huu hivyo kuwafanya wawe na kiu ya kutaka kumuona mtoto huyo wa pekee wa Kiba kwa mkewe Amina Khalef.
“Mashaallah hongera sana… tuoneshe sura tumuone jamani mwanetu…Hongera sana baba #KEYAAN…Mabaharia wangapi tunaenda na sisi kuoa nje ya nchi? Tujuane,” hayo yalikuwa ni baadhi ya maoni ya mashabiki wa Kiba huko Instagram.
HABARI MPYA SASA…
Kwa mujibu wa chanzo ambacho kipo karibu na familia ya Kiba, Keyaan atafanyiwa sherehe kubwa baada ya kutanguliwa na kisomo maalum (Hakika) hivi karibuni ambayo itahudhuriwa na baadhi ya mastaa wachache ambao watapewa mwaliko maalum.
“Yaani ishu itakuwa kubwa kwa sababu safari hii Kiba anataka kufanya kitu cha tofauti kidogo. Hajaweka wazi eneo husika, lakini ni jambo ambalo anataka kulifanya kama sapraizi,” kilisema chanzo hicho.
MIPANGO CHINI KWA CHINI
Chanzo hicho kiliweka wazi kuwa, mipango yote inaendelea kusukwa chini kwa chini hivyo muda muafaka utakapofika, mashabiki wa Kiba, ndugu, jamaa na marafiki wataweza kujumuika pamoja katika sherehe hiyo.
MAMILIONI YATENGWA
“Hapo itakuwa ni kula na kunywa, vyakula vitakuwa vya kutosha, yaani ile fulu mazagazaga. Bajeti nimeichungulia ni ya mamilioni na tayari yameshatengwa mahususi kwa ajili ya tukio hilo baab’kubwa.
“Yaani hapa tunasubiri tu mzee baba Kiba atutajie tu eneo na siku husika, basi tukafanye yetu.
“Suala la watu kula na kunywa si la kitoto, watu watacheza na kuimba pamoja na Kiba katika hafla hiyo, yaani itakuwa siyo sherehe kama hizi za kawaida tulizowahi kuziona kwa watoto wengine wa mastaa,” kilieleza chanzo hicho.
CHANZO CHAZIDI KUTIRIRIKA
Kikizidi kufunguka chanzo hicho kiliweka bayana kuwa, mbali na vyakula na vinywaji, tayari kuna kituo kikubwa cha televisheni kimeshaonesha nia ya kudhamini shoo hiyo hivyo kama mambo yatakwenda vizuri, basi kituo hicho pekee ndiyo kitakuwa na haki miliki ya kurusha tukio hilo.
“Huyu ni mtoto wa staa bwana, lazima afanyiwe kitu fulani cha tofauti hivyo siku hiyo mambo yatakuwa ni kuruka laivu hivyo vyombo vingine havitakuwa na haki ya kurusha labda wakubaliane na hao walionunua haki miliki,” kilisema chanzo hicho.
KIBA ANASEMAJE?
Jitihada za kumpata Kiba ili aweze kutoa utaratibu mzima wa tukio hilo la aina yake hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita muda mrefu bila kupokelewa.
MENEJA WAKE ATOA NENO
Gazeti la Ijumaa lilijaribu kumvutia waya mmoja wa mameneja wa msanii huyo, Aidan Seif ambapo alipopatikana na kuulizwa kuhusu sherehe hiyo alimtaka mwanahabari wetu kuwa na subira kwani ndiyo kwanza wapo bize na maandalizi na mambo yatakapokuwa sawa, kila kitu kitawekwa wazi.
“Wewe tulia kwanza mambo mazuri hayahitaji haraka. Kuna vitu lazima tuviweke sawa na Kiba kabla ya kufanya si unajua Kiba anafuata misingi ya dini hivyo kuna taratibu za kidini lazima zifuatwe katika jambo hilo, muda ukiwa tayari tutakujuza,” alisema Aidan.
FAMILIA YA KIBA
Keyaan ni mtoto wa nne na mtoto wa kwanza wa Kiba kuzaa baada ya kufunga ndoa na Amina.
Kabla ya kufunga ndoa, Kiba alishajaliwa kupata watoto wengine watatu kwa wanawake tofauti; Amaya, Sameer, Samira.
Stori: ERICK EVARIST, IJUMAA
Comments are closed.