The House of Favourite Newspapers

Kasi ya rais Magufuli yabaini vyeti feki 219

0

1Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.

Kasi ya Mawaziri wa Rais John Pombe Magufuli kufanya ziara za kushtukiza na kutoa maagizo kwa watendaji imeanza kufumua uozo baada ya jana kubainika kuwa watumishi 219 kati ya 704 wa serikali wameajiriwa kwa vyeti vya kughushi.

Sakata hilo liliibuliwa baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kutembelea Idara,vitengo vya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi) na kuagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote waliobanika kutumia vyeti visivyo vyao kupata ajira serikalini.

“Watumishi wote waliobainika kupitia Mfumo Shirikishi wa Malipo ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (Payroll), kwamba wametumia vyeti visivyo halali wachukuliwe hatua stahiki,” amesema Kairuki.

Amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa RasilimaliwatuUtumishi, Emmanuel Mlay kutafuta ufumbuzi wa kumaliza tatizo la watumishi wanaotumia vyeti vya kughushi.

“Muwasilishe vyeti vyao Baraza la Mitihani kwa ajili ya uhakiki na baada ya uhakiki muwachukulie hatua stahiki watumishi wanaoonekana kutumia vyeti visivyo halali kwao,” alisisitiza.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa RasilimaliwatuUtumishi, Leonard Mchau, alisema kuwa Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, imehakiki watumishi 704 na kati ya hao, watumishi 219 baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani, waligundulika waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi.

Hata hivyo, Mchau aliongeza kuwa baadhi ya watumishi hao waliobainika kughushi vyeti ili kujipatia ajira serikalini, wamekimbia vituo vyao vya kazi. Mchau aliwaasa wananchi kuepuka mchezo wa kughushi vyeti, ili kujipatia ajira Serikalini.

“Ni kosa la jinai kughushi vyeti kwa lengo la kujipatia kazi, sasa endapo utagundulika umeghushi vyeti, utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” alifafanua Mchau.

Kwa sasa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma inaendelea na uhakiki wa vyeti kwa watumishi wote wa umma nchini mpaka kila mmoja atakapohakikiwa.

Leave A Reply