Usher Raymond: Sijafuta Picha, Akaunti Yangu Imedukuliwa
Staa wa muziki kutoka nchini Marekani, Usher Raymond amejitokeza na kueleza kuwa akaunti yake ya mtandao wa X imedukuliwa na kwamba sio yeye aliyefuta picha zote kwenye akaunti hiyo kabla ya kuifuta akaunti na baadaye kuirudisha.
Usher amejitokeza muda ambao kumekuwa na gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii tangu jana Jumapili, ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakimshutumu kwamba amefuta picha zote na akaunti yake kwa sababu ya kutaka kupoteza ushahidi kuhusiana na sakata linaloendelea kwa swahiba wake mkubwa, Sean ‘Diddy’ Combs.
Tangu Diddy alipokamatwa siku kadhaa zilizopita, watu mbalimbali wamekuwa wakimnyooshea Usher vidole kwani ameishi kwa karibu kwa muda mrefu na Diddy na wengine kumtuhumu kwamba huenda alikuwa akishirikiana na Diddy kwenye tuhuma zinazomkabili.
Uhusiano kati ya Usher na Diddy umedumu kwa miongo kadhaa, kwani Combs alikuwa mtayarishaji mkuu wa albamu ya kwanza ya Usher ya 1994, Usher; na aliishi na Diddy akiwa kijana huku akijifunza biashara ya muziki tangu miaka ya 1990.
Hata hivyo, licha ya Usher kueleza kuwa akaunti yake hiyo ilikuwa imedukuliwa, bado baadhi ya watumiaji wa mitrandao ya kijamii, wameendelea kuonesha mashaka kutokana na majibu yake.