The House of Favourite Newspapers

Yitzhak Rabin: Waziri Mkuu wa Israel Aliyeuawa Kisa Kutaka Amani na Wapalestina

0
 Kutoka kushoto, Rabin, Bill Clinton na Yasser Arafat

Kama kuna watu ambao wangeweza kuumaliza kabisa mgogoro kati ya Israel na Palestina, ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin na aliyekuwa kiongozi wa Palestina, Yasser Arafat.

Septemba 13, 1993, Rabin na Arafat walifanya mazungumzo marefu na ya siri katika Ikulu ya White House ambayo yalisimamiwa na wanadiplomasia wa Norway. Mazungumzo hayo yalipewa jina la Oslo Accord au Mkataba wa Oslo na lengo lake kubwa lilikuwa ni kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miaka mingi kati ya Israel na Palestina.

Pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya Palestina kuitambua Israel kama taifa huru, na Israel kuondoka kwenye eneo la Palestina Ukanda wa Gaza ililokuwa ikilikalia kimabavu, hatua ambayo ingewezesha Palestina kujitawala katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi katika Mji wa Jericho.

Masuala mengine ya msingi kama makazi ya Wayahudi kwenye ardhi inayokaliwa, mustakabali wa Wapalestina waliofanywa wakimbizi mwaka 1948 na hatma ya Jerusalem, yaliachwa bila uamuzi.

Hatua hiyo ilikuwa inakwenda kumaliza kabisa uhasama wa miaka mingi kati ya Wayahudi na Wapalestina.

Hata hivyo, baadhi ya Waisrael, hasa wenye misimamo mikali, hawakupendezwa na hatua hiyo na kuona ni kama Rabin alikuwa amewasaliti wa Israel kwa kukubali kuondoka kwenye makazi ya Gaza na kuwaachia Waisrael.

Ni hapo ndipo njama za kutaka kumuua Rabin zilipoanza.

Jioni ya Novemba 4, 1995, Rabin alikuwa akihutubia kwenye mkutano mkubwa katika Uwanja vya Kings of Israel Square (sasa unaitwa Rabin Square) jijini Tel Aviv, ambao ulifanyika kwa lengo la kuunga mkono Mkataba wa Oslo.

Mkutano ulipomalizika, Rabin alitembea akishuka ngazi kuelekea kwenye mlango wa gari lake, ghafla risasi tatu zikafyatuliwa na kijana ambaye alikuja kutambulika kuwa ni Yigal Amir, kijana mdogo wa Kiyahudi aliyekuwa na msimamo mkali.

Risasi mbili zilimpiga Rabin, na ya tatu ilimjeruhi kidogo Yoram Rubin, mmoja wa walinzi wa Rabin. Rabin alipelekwa Hospitali ya Ichilov iliyo karibu, ambako muda mfupi baadaye, Rabin alifariki dunia kwenye meza ya upasuaji kutokana na kupoteza damu nyingi na mapafu mawili kuharibiwa na risasi.

Huo ukawa mwisho wa mkataba wa Oslo wa kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

Mwandishi: @hashpower7113

Leave A Reply