Wanaofukuzwa Marekani Hatarini Kupelekwa Magereza Hatari

Serikali ya Marekani imefikia makubaliano ya ajabu na Serikali ya El Salvador ambayo yatairuhusu nchi hiyo kupokea wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Marekani wenye uraia wa nchi yoyote, ikiwa ni pamoja na wahalifu hatari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Rais wa El Salvador, Nayib Bukele, amekubali makubaliano haya yasiyo na kawaida katika historia ya uhamiaji duniani.

“Bukele amekubali pia kuwachukua wahalifu hatari waliopo magerezani Marekani, hata kama ni raia wa Marekani au wakazi wa kudumu,” Rubio alisema.
Katika mkutano uliofanyika jana Jumatatu Feb 3, serikali ya Bukele iliahidi kurejesha wanachama wa genge la MS-13 kutoka Marekani, pamoja na wahamiaji haramu wenye rekodi za uhalifu kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Venezuela na kundi la wahalifu la Tren de Aragua.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tammy Bruce, alisema: “Katika hatua ya kipekee ambayo haijawahi kushuhudiwa, Rais Bukele ameahidi pia kuwahifadhi magerezani mwake wahalifu hatari wa Marekani, wakiwemo raia wa Marekani na wakazi wa kudumu.”
Rubio alikuwa nchini El Salvador kama sehemu ya ziara yake ya mataifa matano ya Amerika ya Kati, akilenga Costa Rica, Guatemala, na Jamhuri ya Dominika, huku suala la uhamiaji likiwa ajenda kuu.