The House of Favourite Newspapers

Hata Malinzi wa BMT naye ni jibu tu, kabisa anastahili kutumbuliwa

0

 

Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nnape Nnauye alitangaza kutengua utezi wa aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Henry Lihaya.

Nnape alieleza kutofurahishwa na utendaji wa kiongozi huyo ambaye amekaa BMT kwa miaka saba. Maana yake hakuwa mtendaji mzuri au hakufanya vizuri majukumu yake.

Wakati Lihaya anaondoka, naona Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi anaendelea kubaki na amepewa kazi ya kuteua katibu mtendaji mwingine ambaye anaamini ni mchapakazi.

Kwanza nianze hivi, ninauunga mkono kabisa uamuzi huo wa Waziri Nape kwa kuwa sasa tunatakiwa mabadiliko makubwa katika michezo.

Tukubali waungwana, mwendo na mwenendo katika michezo umekuwa ni wa kusuasua sana kwa kuwa watu hawako makini na bado wana yale mawazo ya kizamani kabisa kwamba michezo ni kitu cha ziada.

Miaka 10 nyuma, hata serikali iliamini michezo ni kitu cha kujifurahisha tu. Hakukuwa na maana ya kukitilia maanani lakini leo utaona mambo ni tofauti.

Hata kama serikali ingekuwa haitaki, inalazimika kufanya hivyo. Leo inachukua kodi kutoka michezoni, inasaidiwa upatikanaji wa ajira, inasaidiwa katika suala la kupunguza vijana kuvuta unga na mambo mengine ya uhalifu. Michezo inaliwakilisha taifa na wakati mwingine kulipa sifa.

Kama ni sekta muhimu, tukubali ikitiliwa maanani na kuongozwa kwa jicho la wanaotaka mafanikio, nchi yetu itafaidika na kufaidisha wananchi wengi kwa furaha na hata kipato.
Sasa watu wanaotakiwa mfano kuongoza baraza la michezo kama BMT, hawapaswi kuwa wale wanaofanya kama vile sehemu ya burudani. Mfano Mwenyekiti wa BMT, Dionis Malinzi ambaye ni mfanyabiashara mkubwa.

Sijawahi kuona ubunifu wake, sijawahi kuona anasimama na kusema jambo akasimamia utakelezaji. Kama kweli Nape aliona Lihaya alilala, basi bosi wake alilala zaidi yake.

Utaona hadi waziri anakwenda kumuondoa Lihaya kwa kuonekana hakuwa mtendaji sahihi lakini Malinzi hakuwahi kueleza kutoridhishwa kwake na wanamichezo wakajua. Kama alisema labda hawezi kumng’oa, mbona hatujawahi kusikia hata amefanya jambo lililoleta mabadiliko katika vyama vya michezo.

Yanayofanyika ni yaleyale ya enzi zile. Ninaamini ana kazi nyingi sana za kibiashara na BMT huenda ni kama sehemu ya kuburudika tu kwake. Huu ndiyo wakati mwafaka akae kando.

BMT inatakiwa kuingia kuleta mabadiliko. Inatakiwa BMT ya wabunifu na wenye nia ya kusaidia michezo ya Tanzania na si hii ya sasa chini yake.

Mara kadhaa nimehoji mara nyingi kuhusiana na BMT, hata yale makato kutoka katika mechi za soka, yanakwenda BMT kwa sababu ipi na yenyewe inaifanyia nini michezo.

Kama ilivyo kwa ule mfuko wa maendeleo ya michezo. Ambao umekuwa ukichota tu fedha na hatujui unafanya nini au kwa msimu uliingiza kiasi gani.

Nilikuwa nikilia na wale watendaji wa wizarani, mfano aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo. Nilikuwa nikiwaona wakati timu inakabidhiwa bendera, au kuna hafla watakuwa wamealikwa kama wageni rasmi au wameenda pale kwa kuwa waziri yuko pale.

Nape ameamua kuwasimamisha, yeye amekuwa shujaa ambaye hajakata kona wala kuingia woga. Ninaamini alipoanzia ni njia nzuri na huenda ikawa ni sehemu ya mabadiliko ya michezo lakini kama wengi mtamuunga mkono.

Kuanza upya si ujinga, ikiwezekana Malinzi naye atumbuliwe, apumzike na kupisha wengine ikiwezekana atakapokuja mtendaji mpya, basi akutane na mwenyekiti mpya ili waanze pamoja.

Leave A Reply