The House of Favourite Newspapers
gunners X

Serikali Yajikiti Kuboresha Mfumo Wa Utoaji Gawio

0

Ofisi ya Msajili wa Hazina (Tanzania) imeshiriki kikao cha wadau cha kuwasilisha Rasimu ya Muongozo wa Uandaaji wa Sera ya Gawio kwa taasisi za uwekezaji wa umma Zanzibar.

Kikao hicho, kilichofanyika Jumanne, Novemba 11, 2025, katika ukumbi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA), Zanzibar, kilifunguliwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Bw. Aboud Hassan Mwinyi.

Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Kaimu Msajili wa Hazina Tanzania, Bi. Lightness Mauki, alisema hatua ya kuandaa Muongozo wa Sera ya Gawio ni sehemu muhimu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha taasisi za umma na zile zenye uwekezaji wa Serikali zinatoa mchango chanya katika uchumi wa nchi.

Alibainisha kuwa sera hiyo inalenga kuweka mfumo unaoeleweka, wenye uwiano na haki katika utoaji wa gawio, ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa mitaji ya umma.

Bi. Mauki, aliyeongozana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Chacha Marigiri, alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni, bado kuna changamoto kwa baadhi ya taasisi ambazo hazijatekeleza ipasavyo wajibu wao wa kutoa gawio.

“Uwazi, ushirikiano, na nidhamu ya kifedha ni mambo muhimu yatakayosaidia kuboresha mwenendo wa utoaji wa gawio kwa taasisi zote za umma,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Bw. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha taasisi na mashirika ya umma yanafanya vizuri katika utoaji wa gawio, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kikao hicho kiliwahusisha wakuu wa taasisi za uwekezaji wa umma pamoja na watendaji wa Idara ya Mitaji ya Umma na Uwekezaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar.

Pia kilihudhuriwa na Msajili wa Hazina Zanzibar, Bw. Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, ambaye aliongoza timu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar katika majadiliano hayo.

Bw. Sanya alisema serikali ina dhamira ya kuhakikisha taasisi zote za umma zinakuwa na utendaji wenye tija, unaowezesha serikali kupata gawio litakalotumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Mashirika na taasisi za umma ni injini muhimu katika uchumi wa taifa. Ni wajibu wetu kuhakikisha zinafanya vizuri kibiashara na kutoa gawio stahiki ili kuchangia maendeleo ya wananchi,” alisema.

Leave A Reply