The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi-72

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Watu wengine waliwaona polisi kuwa wazembe mno, hawakuamini kama katika kipindi chote hicho hawakufanikiwa kumpata Dickson. Aliwakimbia katika mazingira ya kutatanisha sana hali iliyomfanya IGP Mayala kukasirika mno.

Alichokiona kwa polisi wake ni kwamba walikuwa wazembe, aliwaamini, alijua kwamba walikuwa wachapakazi wakubwa lakini swali likaja ni kwa namna gani huyo Dickson aliweza kuwatoroka, yaani kutoka ndani ya Jiji la Dar es Salaam pasipo kugundulika?

Hilo ndilo lililomfanya kuzungumza na kitengo cha upelelezi na kumhitaji mpelelezi mmoja, mwenye uwezo mkubwa ambaye angekula sahani moja na Dickson mpaka kuhakikisha mtu huyo anakamatwa.

Walijua ni mtu gani waliyekuwa wakishughulika naye, hakuwa mtu mzuri hata kidogo, kama kupambana, hata kama ungemuwekea watu watano, angeweza kupambana nao na kuwapiga wote hivyo hata mpelelezi ambaye alitakiwa kutumwa kwenda kumtafuta, alitakiwa kujua jinsi ya kupambana ili iwe rahisi kumtia nguvuni.

“Tumchukue James Malope…” alisema polisi mmoja.

“Unahisi ataweza?” aliuliza IGP Mayala.

“Nadhani…”

“Hatua tuliyofikia sasa hivi si ya kudhani, tunahitaji watu wenye uhakika, unahisi ataweza?” aliuliza IGP Mayala.

“Ataweza tu.”

“Hapana! Bado sijafikiri hilo, nadhani Fredrick Limao atafaa zaidi kwa kuwa ndiye mtu mwenye uwezo mkubwa katika masuala ya upelelezi,” alisema IGP huku akionekana kuwa na uhakika na kile alichokuwa akikisema.

“Hakuna tatizo mkuu,”

Fredrick Limao alikuwa mpelelezi kutoka TISS ambaye kwa kipindi hicho alikuwa ametoka nchini Urusi alikopelekwa kwa ajili ya kumtafuta mtu aliyejulikana kwa jina la Mirkovic Ilalatovic.

Huyo alikuwa mfanyabisahara mkubwa wa madawa ya kulevya. Aliua watu na kujificha huku nyuma yake kukiwa na ulinzi madhubuti. Hakupatikana kirahisi, Wamarekani na watu wao wa upepelezi wa kimataifa, CIA walijaribu kumtafuta kwa kipindi cha miaka mitano, hawakufanikiwa kumpata.

Tofauti na CIA, hata shirika la Kijasusi la Urusi, KBG nalo lilijaribu kumtafuta kila kona lakini halikufanikiwa. Mara baada ya kuhangaika sana, walichokifanya KGB ni kuomba msaada kutoka Afrika Kusini ambapo ikatuma wapelelezi wake waliokaa huko kwa muda wa miaka miwili lakini waliambulia patupu.

Mirkovic aliendelea kuwa gumzo, bado watu wengi walikuwa wakiuawa kila siku. Madawa ya kulevya yalisafirishwa, hongo ilitapakaa kwa kila polisi aliyekuwa akiwakamata wasafirishaji wa madawa hayo, kwa wale waliokataa kupokea hongo hiyo, waliuawa wao na familia zao.

Hofu kubwa ikatanda na hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumpata mtu huyo. Baada ya miaka kadhaa kukatika, hatimaye akatumwa mtu mmoja, aliyepokea mafunzo ya kijasusi kutoka nchini Cuba, huyo alikuwa Fredrick Limao.

Kwa watu wengi walihisi kwamba hiyo ingekuwa kazi kubwa sana ila moyoni mwake, kazi hiyo ilionekana kuwa nyepesi mno na wala isingemchukulia muda wake mwingi.

Alipofika nchini Urusi, kitu cha kwanza kabisa akajifanya mwanachuo katika Chuo Kikuu cha Moscow, hakukuwa na mtu aliyeelewa kilichokuwa nyuma ya pazia.

Huko chuoni, akakutana na kijana aliyeitwa Paul Mirkovic, akalazimisha urafiki na kwa sababu alikuwa na akili sana, hatimaye akafanikiwa, wakawa marafiki wakubwa, wakaaminiana na hatimaye kuanza kuambiana mambo yao ya siri.

“Wewe ni rafiki yangu mkubwa sana Limao…” alisema Paul huku akimwangalia Fredrick.

“Najua hilo!”

“Kuna kitu nataka kukwambia..”

“Kipi?”

“Unaweza kutunza siri?”

“Naweza, kwa nini nisiweze…”

“Basi sawa! Baba yangu ni miongoni mwa watu wenye fedha nyingi hapa Urusi. Kutokana na fedha hizo ana mali kibao na kuheshimiwa sana,” alisema Paulo.

“Hongera kwa kuwa na baba mwenye fedha nyingi, nini chanzo cha fedha hizo?” Fredrick alimwuliza.

Paulo alipoulizwa hivyo, alicheka na kumwambia siku zote mjini ni mipango.

“Unaposema mjini ni mipango nashindwa kuelewa, au biashara zake hazieleweki?” Fredrick alimwuliza.

“Wewe elewa ana ishu kubwa zinazomwingizia fedha usiku na mchana, huwa nakutana naye kila siku ya Jumamosi katika klabu ya Amazon…” alisema Paul.

“Baba yako nani? Mzee Mirkovic?”

“Ndiyo!”

“Mmh! Mimi mbona simjui!”

“Ni mtu maarufu sana hapa Urusi, huyo ndiye ninayekutana naye, kuna siku utamuona tu,” alisema Paul.

Kazi kubwa aliyokuwa nayo, ikarahisishwa, hakuamini kama ingekuwa nyepesi kiasi hicho. Alichokifanya baada ya mwezi mmoja ni kuwataarifu polisi kisha mtu huyo hatari kukamatwa.

Baada ya kufanya kazi hiyo na nyingine nyingi za hatari, hatimaye akaamua kurudi nchini Tanzania huku akiwa na heshima kubwa. Alipofika, hakukaa sana akaambiwa kulikuwa na kazi ya kufanya, kumtafuta mtu aitwaye Dickson aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam.

Alipoambiwa, kwake haikuwa kazi kubwa. Kama aliweza kupambana na Wazungu, wenye uwezo mkubwa angeshindwa vipi kwa Mtanzania, tena kwa mtu kama Dickson? Kila alipojifikiria, kwake, kumtafuta mtu huyo ilikuwa kazi nyepesi kabisa, yaani ni kama kumsukuma mlevi kwenye mremko wa mlima. Akakubali, akajipanga na kuanza kazi ya kumtafuta mtu huyo hatari.

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma mwendelezo wa hadithi hii           ya kusisimua wiki ijayo.

Leave A Reply