MUME AFUATA PESA YA KITOWEO ATM… ARUDISHWA AKIWA MAITI!

UCHUNGU wa kufiwa na mume uliyeachana naye muda mfupi baada ya kukuambia kuwa anatoka kidogo kufuata fedha za matumizi kwenye mashine ya ATM, halafu akarudishwa maiti usiombe ukufike!  

 

Simulizi ya Habiba Adam mkazi wa Mwandege, mkoani Pwani aliyefiwa na mumewe katika mazingira ya kutatanisha inahuzunisha. “Januari 12 mwaka huu, mume wangu aitwaye Omari Magonga (35) aliniaga kuwa anatoka kidogo kwenda kuchukua hela ATM ya matumizi na kitoweo, nikamruhusu,” alisema Habiba.

 

Baada ya ruhusu hiyo, Omari anadaiwa kuondoka kwenda sehemu aliyoiombea ruhusu kwa mkewe huku akimwacha mwanadani wake akisubiri kurejea nyumbani. Ingawa inaelezwa na mke wake kuwa siku hiyo marehemu Omari hakutoka nyumbani kwake na kwamba alishinda na familia yake lakini mtoko wake wa kufuata fedha ulianza kuzua hofu baada ya sekunde, dakika na saa kukatika bila mume huyo kurejea.

 

Hata hivyo, wakati mume wake akiwa ametoka, Habiba alipigiwa simu na wifi yake aitwaye Sauda Abdulhaman; yaani dada wa mumewe akimtaarifu kuwa anakwenda kumtembelea ambapo alimkaribisha. Wakiwa mtu na wifi yake katika kumsubiri Omari arudi toka saa 12 jioni alipoondoka hadi saa 2 usiku hakukuwa na dalili ya kurejea kwake.

 

“Nilipoona kimya kinazidi kwa mume wangu ikabidi nimpigie simu kumuuliza yuko wapi? Akaniambia anamsubiri ndugu yake anaitwa Dula, kuna hela anamletea, akizichukua muda si mrefu atarudi nyumbani,” alisema Habiba. Aidha Omari anadaiwa kuzidi kumsubirisha mkewe kwa bashasha kutokana na kumuuliza kuwa atakapokuwa anarudi nyumbani ampelekee nini mwandani wake kitakachomfurahisha.

 

Habiba alimjibu mumewe: “Niletee chochote tu mume wangu nitashukuru.” Saa nne usiku ilifika bila Omari kuonekana, dada yake alimpigia simu kumuuliza kulikuwa na tatizo gani mbona harudi nyumbani ambako familia inamsubiri? Majibu ya kaka yake yalikuwa: “Dada nakuja usiondoke kama ni kulala unaweza kulala hapo kwa wifi yako.” Subira waliyokuwa wameambiwa wawe nayo ikaanza kuyeyuka ambapo mke na dada yake waliamua kuingia ndani kulala huku wakiendelea kumsubiri Omari arudi.

Kama wasemavyo Waswahili usingizi hauna adabu, walipoingia vyumbani walipitiwa hadi saa tisa usiku ambapo jambo jipya lilijitokeza. Mke wa marehemu anaendelea kusimulia: “Mida ya saa tisa usiku, ikaingia meseji kwenye simu yangu nikaipuuzia. “Muda mfupi ikaingia nyingine ya pili nikaangalia ile namba ni namba ya rafiki yake na mume wangu.”

 

Aliongeza kuwa, alipoisoma meseji hiyo ya pili ilikuwa ina ujumbe uliokuwa ukimtaarifu kuwa mume wake amepata majanga. Majanga gani? Swali lilikuwa halina majibu ambapo mke huyo wa marehemu Omari aliamua kupiga simu kuuliza kilichomfika mumewe. “Nilipompigia simu nikamuuliza amepata majanga gani?” alisema Habiba na kuongeza kuwa alijibiwa, “hebu subiri kidogo nitakupigia.”

 

Muda wa kusubirishwa kuhusu majanga yaliyompata mume wako huambatana na hofu, taharuki na maswali mengi jambo ambalo lilimfanya mke huyo wa marehemu kushindwa kuvumilia na kuamua kumtafuta ndugu wa marehemu (Dulla) aliyetajwa awali kuwa Omari alikuwa akimsubiri ampelekee fedha.

 

“Ikabidi nimpigie simu Dulla hakupokea, ikabidi nipige namba ya mke wake bahati nzuri akapokea mwenyewe Dulla. “Nikamuuliza, shemeji uko wapi? akaniambia mimi nipo nyumbani mbona saa hizi usiku vipi shemeji? Nikamwambia wewe leo umekutana na ndugu yako? akanijibu ndiyo nilikutana naye, nikamwambia saa ngapi akasema nilikutana naye mida ya saa nne usiku lakini baadaye niliachana naye,” alisema Habiba akikaririsha mazungumzo aliyokuwa akiongea na Dulla.

 

Katika hatua nyingine ilifahamika kuwa baada ya Dulla kuachana na ndugu yake Omari alikuwa na ndugu yake mwingine mwingine anaitwa Maleta. “Ikabidi nimpigie shemeji yangu Maleta nikamuuliza shemeji upo na ndugu yako hapo akaniambia nimeachana naye mida ya saa tano usiku hivi, nikamwambia ulivyoachana naye yeye kaenda wapi?

 

“Akaniambia yeye alirudi nyumbani kwake na mume wangu (Omari) alimwambia anarudi nyumbani. Nikamwambia mimi mbona nimetumiwa meseji inasema amepata majanga, sijui ni majanga gani. “Shemeji yangu ikabidi aniambie ukweli kwamba alipoachana naye muda mfupi alipigiwa simu kuwa mume wangu amepata ajali, amegongwa na pikipiki,” alisimulia Habiba.

 

Aliongeza kuwa baada ya kuendelea kumdadisi shemeji yake Maleta, alimwambia kuwa alipokwenda kumfuata Omari alimkuta akiwa amelala chini huku damu zikimtoka ambapo alimchukua na kumpeleka Hospitali ya Zakhiem, Mbagala jijini Dar es Salaam. Baada ya kuambiwa hivyo, mke huyo wa marehemu aliwaamsha majirani ambao waliongozana naye hadi hospitalini ambako walifika na kuambiwa kuwa mgonjwa kahamishia Hospitali ya Temeke.

 

“Wakati tunakwenda Temeke (hospitalini) kuna simu ya shemeji yangu mwingine ikanipigia na kuniambia kuwa nirudi nyumbani kwa sababu mgonjwa haruhusiwi kuonwa na mtu yeyote. “Tulipofika nyumbani wakanipa tu taarifa kwamba mume wangu tayari ameshafariki, amechomwa na kisu mbavuni,” anasimulia Habiba.

 

Safari ya Omari kutoka ATM kuchukua fedha za matumizi hadi kuchomwa kisu na kupoteza maisha imejaa maswali mengi lakini mashuhuda wanasema kuwa alipatwa na mkasa huo akiwa eneo la Bombani kulikuwa na muziki wa Singeli. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa marehemu baada ya kumaliza mizunguko yake aliongozana na baadhi ya ndugu zake kwenda kwenye muziki ambako unadaiwa kutokea ugomvi uliosababishwa na mwanamke mmoja ambaye hakujulikana.

 

“Wakiwa huko kwenye muziki kuna msichana alikuwa kama anagombewa na kundi la wahuni sasa marehemu Omari alipokwenda kutaka kama kumuokoa kwenye sakata hilo ndiyo akachomwa kisu na kufariki dunia,” kilieleza chanzo chetu. Hata hivyo haikufahamika nani alimchoma kisu, sababu yake nini na marehemu iikuwaje aende kuingilia kasheshe hiyo ya wahuni.

 

Kutokana na utata huo ndugu wa marehemu akiwemo mke wake wameviomba vyombo vya usalama kuharakisha uchunguzi ili haki iweze kutendeka. “Serikali itusaidie tuweze kuwapata wahusika, maana mume wangu kaniachia watoto wawili wadogo ambao wanasoma; nashindwa kwa kweli hata pa kuanzia kuwalea wanangu,” alisema kwa masikitiko mke wa marehemu.

 

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Chatembo kulipotokea mauaji hayo, Salum Mkumba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Taarifa ya kwanza niliipata baada ya kupigiwa simu na Polisi Jamii kwamba kuna kijana ameuawa mtaani kwangu na kulikuwa na muziki. “Niporudi tulienda eneo la tukio na kufanya taratibu za kimtaa, lakini kwa kuwa polisi wanafanya uchunguzi tusiwaingilie, tuwaachie wafanye kazi yao,” alisema mwenyekiti huyo.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment