A-Z Harmonize kuzabwa kofi
DAR: Video inayosambaa mitandaoni ikimuonesha staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ akizabwa kofi na shabiki wake, imekuwa gumzo, IJUMAA linakupa A-Z. Harmonize au Harmo alikaripiwa na shabiki huyo aliyempandia jukwaani alipokuwa akipafomu mjini Sumbawanga hivi karibuni. Hata hivyo, kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, shabiki huyo alikiona cha moto kutoka kwa mabaunsa wa Harmo.
Tukio hilo lilijiri wiki chache baada ya shabiki mwingine kumshikilia kwa nguvu na kukataa kumwachilia alipokuwa akipafomu kwenye Viwanja vya Mwembe- Yanga jijini Dar. Kwa mujibu wa mashabiki wa Harmo waliozungumza na IJUMAA, Harmo na uongozi wake wanapaswa kuimarisha ulinzi kwa staa wao au kuangalia upya uhusiano wake na mashabiki wake.
ILIKUWAJE?
Katika video hiyo ambayo Harmo anaonekana akizabwa kofi huku akitumbuizia umati, shabiki huyo alirukia jukwaa na kumfuata moja kwa moja mwimbaji huyo wa Wimbo Uno. Shabiki huyo alipomfikia Harmo, alionekana kama anabishana naye kabla ya kumzaba kofi na kudhibitiwa na mabaunsa na kujikuta akiruka na kurejea kwenye umati wa mashabiki.
Tukio lingine liliacha maswali, wakati Harmo akitumbuiza jijini Mwanza hivi karibuni, alishindwa cha kufanya baada ya shabiki kumrukia jukwaani ambapo ilibidi itumike nguvu kubwa kumdhibiti ingawa hakumfikia Harmo.
Hata hivyo, Harmo amekuwa akitamba na kuwasifia mabaunsa wake kwenye Instagram. Tukio lingine lenye sura tata la kukumbukwa ni pale walinzi walipolazimika kumdhibiti shabiki, alimvamia Harmo na kumshika mguu mbele ya Rais Dk John Pombe Maguli ‘JPM’. Ilikuwa Novemba, mwaka jana.
Katika tukio hilo, iliwalazimu walinzi waliokuwepo kuingilia kati na kumuondoa jamaa huyo na kumruhusu Harmo kuendelea kutumbuiza mbele ya JPM.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA juu ya matukio hayo, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ ambaye alisema, wengi wao ni mashabiki wanaokuwa na mzuka juu ya msanii wao. “Hawana lengo baya, wengi wao wanashindwa kujizuia kutokana na mapenzi waliyonayo kwa msanii wao.“Wanampenda sana. Kila kona anapokwenda, mashabiki hupenda angalau kumgusa tu ili wafurahi,” alisema Beauty.
Stori: NEEMA ADRIAN, Ijumaa