The House of Favourite Newspapers

Aaiii… Wewee…!

0

Sanura alikaa beneti na Msoba wakizungumza kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi huku kila mmoja akionesha hisia za upendo kwa mwenzake, hususan kwa kuwekeana wazi kwamba wanapendana…

“Baby unajua kama mimi nakupenda sana?” Sanura alimwambia Msoba…
“Dear hata mimi nakupenda sana mpenzi wangu, we unajua,” alidakia Msoba…
“Basi tudumishe mapenzi yetu, tuishi kwa kupendana kama mke na mume ili tuje tufikie kwenye kulea familia,” alisema Sanura huku akimkamatakamata mwanaume huyo sehemu mbalimbali za mwili, hususan kifuani kwenye eneo la ‘bustani’.

Sanura ni mwanamke aliyeolewa kwa ndoa ya msikitini, lakini walitengana na mumewe, Jalia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya yeye mwanamke kudaiwa kuwa mchepukaji wa kupitiliza.
Baada ya kuachana na Msoba, Sanura alijikuta amenasa kwenye penzi la Msoba.

Msoba yeye pia aliwahi kuwa na mke wa ndoa, Sada lakini wakaachana kwani maisha ya ndoa kwake na mwanamke huyo yalikuwa magumu sana, kiasi kwamba kuna wakati mwanaume alikuwa akilazwa nje.
Hivyo kuwa pamoja kwao kuliwafanya wawe na upendo wa dhati kila mmoja akihisi hakuwa katika chaguo sahihi.

***
Siku moja, katika pitapita zao, Sada alikutana na Jalia, ilikuwa kwenye mgahawa wa Mlima City, walikaa meza mbalimbali, lakini wakajikuta wakisalimiana mwishowe, Sada akahamia kwenye meza ya Jalia.
Katika kuulizana historia, Sada alijianika…
“Nilikuwa na mume wangu wa ndoa, lakini tuliachana mwaka juzi,” alisema Sada…
“Kisa cha kuachana?”

“Ha! Unajua tena, kwenye ndoa ikifika mahali hamuaminiani basi hakuna ndoa hapo.
Jalia naye alisema kwa upande wake kuhusu ndoa…
“Hata mimi, nikuwa na mke wa ndoa lakini tuliachana huohuo mwaka jana…
“Jamani pole! Na wewe sasa kisa kilikuwa nini?” aliuliza Sada…

“Kama wewe tu. Ukiwa na mwenzako halafu akawa haeleweki ujue hakuna ndoa hapo.”
“Pole sana jamani, anaitwa nani?” aliuliza Sada…
“Anaitwa Sanura…wewe jamaa anaitwa nani?”
“Anaitwa Msoba.”

***
Msoba na Sanura walizungumza mengi siku hiyo, wakafika mahali wakakubaliana kwamba, ndani ya miezi mitatu ijayo wawe wamefikia hatua ya ndoa.
“Hilo mimi naliafiki baby maana nakupenda sana,” alisema Sanura, akamkumbatia Msoba mbele za watu ambao walikuwa wamekaa wakiendelea na mambo yao.

***
Sada na Jalia walianza uhusiano wa mapenzi siku hiyo kila mmoja akimhakikishia mwenzake anampenda. Siku hiyo kila mmoja alifika Mlimani City na gari lake kama ilivyo kwa Sanura na Msoba.
Usiku huo, Sanura na Msoba waliutumia kuwa pamoja nyumbani kwa Msoba maeneo ya Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam kama ambavyo Sada na Jalia wao waliutumia kuwa wote hapo Mlimani City!

***
Usiku Sanura akiwa kitandani, Msoba akiwa anaoga, Sada alimkumbuka mtalaka wake huyo, akamtumia meseji hii…
“Za leo? Kuna ile kadi yangu ya gari niliyoitoa fotokopi nikaiweka juu ya kabati, please nitaipataje?”
Kwa vile alikuwa anaoga, Msoba hakusoma meseji hiyo, lakini Sanura alijua kuna meseji imeingia. Kwa hiyo aliporudi alimtonya…

“Baby kuna meseji imeingia kwenye simu yako,” alisema Sanura…
“Oke, sijui atakuwa nani?”

“Sijui baby!” alijibu Sanura kwa sauti yake ndogo sana na tamu.
Msoba aliishika simu yake na kukutana na meseji ya mtalaka wake, akasonya kwanza kisha akasoma.
Alipomaliza alimwangalia Sanura ambaye naye alikuwa akimwangalia baada ya kumsikia amesonya…
“Huyu ni yule mtalaka wangu, anaulizia habari za kadi yake ya gari eti,” alisema Msoba…
“Mh! Kadi ya gari anaulizia leo, mwambie ilipotea,” alisema Sanura akimfundisha Msoba. Palepale Msoba akamtumia meseji…

“Ilipotea.”
Jibu hilo lilimkera sana Sada, akamwambia Jalia…

“Kuna kadi yangu ya gari niliiacha kwa mtalaka wangu, sasa naitaka anasema imepotea, itakuwa kweli au hataki tu kunipa?” aliuliza Sada akiomba ushauri…
“Itakuwa hataki tu kukupa, mtumie meseji, mwambie utakwenda kuitafuta mwenyewe usikie atajibuje?”
Sada alituma meseji…

“Oke, nitakuja mwenyewe kuitafuta,” alituma meseji hiyo kwa Msoba ambaye alicheka huku akiisoma meseji hiyo kwa sauti ili Sanura naye asikie…
“Mwambie umeshaoa siku hizi, hakuna nafasi ya kuingia ndani kwako,” Sanura alimfundisha Msoba jinsi ya kumjibu Sada…
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Itaendelea wiki ijayo.
tuma maoni kwenda kwa mhariri na. 0655 207520.

Leave A Reply