The House of Favourite Newspapers

AANGUSHA BONGE LA PATI KUWASUTA MASHOGA ZAKE

DAR ES SALAAM: Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Rehema Mohammed Mkome ‘Rais wa Charambe’, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam hivi karibuni alizua kioja cha mwaka baada ya kuamua kuandaa bonge mahsusi kwa ajili ya kuwasuta mashosti zake.

Akizungua na Risasi Jumamosi, rais huyo wa Charambe alidai kuwa alitumia kiasi cha shilingi laki tatu na nusu kuandaa sherehe hiyo kulipia mchele kilo 10, nyama kilo 20, video shooting (shilingi elfu sabini) na muziki (elfu hamsini) akidai siku hiyo alikuwa amepania kuwachamba mashosti zake ambao walimtenda mabaya na wao ndio walianza kumchamba kupitia kwenye sherehe ya rafiki yao mwingine ambaye hakumtaja jina. “Wao walianza mimi nikaamua kumalizia namshukuru Mungu watu waliniitika tulichamba kwelikweli,” alisema rais huyo.

CHANZO NI NINI?

Rais huyo alieleza chanzo cha kuwatolea maneno wenzake na kuwafanyia pati maalumu kuwa ni kutokana na urafiki waliokuwa nao kwa muda mrefu kisha wao wakamgeuka na kumuwekea magenge wakati hakuna kosa lolote alilowafanyia.

“Unajua marafiki zangu hao Johari na Asha tulikuwa kundi moja nilipohamia Mbagala tulikuwa tukisaidiana kwa shida na raha lakini siku moja walitokea kugombana kuna mmoja alikuwa akimtuhumu mwenzake kuwa amemchukulia mumewe baada ya kugombana kwao makundi yetu yakapasuka.

“Mimi niliamua kubaki na Asha na Johari akawa na kundi lake tukaendelea na maisha lakini kila siku kukawa na manenomaneno mengi, siku moja alitokea dada mmoja ambaye aliamua kutusuluhisha tukarudi kuwa kundi moja kama kawaida maisha yakaendelea,” alisema rais huyo. Aidha, alisema kuwa baada ya kukaa kwa muda mrefu, wakaanza kugombana tena Johari na mwenzake wakajaribu kuwasuluhisha lakini ikashindikana.

“Sasa siku moja niko kwangu nikasikia wameitwa na mtu wamesuluhishwa akaja mtu akaniambia unajua kuwa wenzako wanasuluhishwa huko ila wewe hawajakuita, mimi nikaona sawa tu kwani nilichokuwa naomba ni hicho,” alisema rais huyo.

Alisema kuwa, baada ya siku kadhaa, wakaandaa sherehe yao bila kumualika lakini kwenye sherehe hiyo ndipo walitumia nafasi ya kumchamba yeye na kila aliyekuwa kwenye sherehe alimwambia kuwa yeye ndio mbaya wao na wamemchamba sana.

“Kitendo hicho kiliniuma sana kwani sikujua kosa langu na hata kunisemesha walikuwa hawanisemeshi kwa lolote lakini mimi niliendelea kuwasalimia nikikutana nao, wikiendi iliyopita Jumapili nilikuwa na sherehe ya mtoto wangu nikaamua kuandaa sherehe tatu ya kufagia uwanja, kuchambua mchele na ya kumpa vyombo vya jikoni ‘kicheni pati’ katika sherehe zangu hizo tatu ndipo nikajiwa na wazo la kuandaa na sherehe hiyo ya kuwalipizia kisasi kwani waliniumiza sana,” alisema rais huyo.

SHEREHE YAVAMIWA NA POLISI

Sherehe hiyo ilivamiwa na polisi ambao walikuwa kwenye doria lakini wapo waliodai kuwa polisi hao walitumwa na upande wa pili ili kuvuruga sherehe hiyo ambapo watu walikimbia na wengine kuumia kwa mbio huku wengine wakiwa wameibiwa simu na vipochi vyao.

“Sherehe ilifana kwelikweli lakini polisi ndio waliharibu kwani walivamia na kuwakurupusha watu ambapo baadhi waliumia na wengine walipoteza simu na vipochi vyao,” alisema shuhuda mmoja aliyefahamika kwa jina la Mama Ali ambaye alikuwa ni mmoja wa waalikwa.

STORI: Hamida Hassan,Risasi Jumamosi

Comments are closed.