Aanika Siri za Chumbani za Mume wa Mtu… Asutwa!

PWANIVituko haviishi duniani! Mkazi wa Vikindu mkoani Pwani anayetajwa kwa jina moja la Shamila ametamani ardhi ipasuke aingie baada ya kuvamiwa na shoga’ke aitwae Khadija Mnanji akiwa na kundi la wasutaji na kuanza kumsuta huku wakimtuhumu kwa kutoa siri za chumbani za mume wa shoga huyo.  Kitimtim hicho kilijiri wiki iliyopita ambapo chanzo chetu cha habari kilisema Khadija alichoshwa na kuzushiwa mambo kila kukicha na shoga’ke huyo wa kupika na kupakua ambapo alifika pabaya kwa kumtolea siri za chumbani za mumewe.

Kiliendelea kueleza kuwa, moja ya mambo yaliyomkera Khadija zaidi ni kitendo cha shoga’ke huyo kumtangazia mumewe kuwa ana busha na kumfananisha yeye na Ambaruti (ingawa haikufafanuliwa kivipi). Katika maisha yao, awali mashosti hao waliaminiana mno na kupeana siri mbalimbali za ndani ikiwa kuombana ushauri mmoja alipokwama, lakini kumbe shosti wake huyo alikuwa akimchora tu.

Baada ya kumpa siri mbalimbali, ilidaiwa kuwa, Khadija alipigwa na butwaa baada ya kugundua kuwa yote aliyokuwa akimweleza shosti wake huyo na kumwambia iwe siri yao, imekuwa si siri tena, bali Vikindu yote watu wanajua. Hali hiyo ilimkera Khadija hivyo akaamua kumfungia kazi shosti wake huyo kwa kumfuata na kundi la wasutaji hadi nyumbani kwake.

“Khadija alitoka na kundi la wasutaji Vikindu-Mtaa wa Zenji na kuandamana nalo kuelekea Mtaa wa Magomeni (hukohuko Vikindu) huku nyimbo, vijembe, vifijo na shangwe za kimbea zikirindima kwenye safari hiyo,” kilisema chanzo. Gazeti la Ijumaa Wikienda, baada ya kutonywa na chanzo kuhusu uwepo wa msuto huo, lilichukua usafiri haraka na kufanikiwa kuwahi eneo la tukio na kukuta mambo yameshakuwa pambe nyumbani kwa Shamila.

Wasutaji hao baada ya kufika nyumbani kwa shosti huyo, kumbe alishawachungulia dirishani na kuwaona ambapo alimtuma mtu awaambie hayupo, lakini alikatishwa tamaa baada ya kuambiwa wasutaji walikuwa wakitaka kutafuta kuni wapike chakula hapohapo ili kumsubiria. Baada ya kusikia hivyo, Shamila aliamua kutoka nje na kuanza kujitetea huku akizungukwa na watu kibao waliokwenda kushuhudia tukio hilo.

Kitendo cha kutoka kilikuwa ni kama amejichongea na kuomba ardhi ipasuke aingie ajifiche, kwani wasutaji hao walianza kumsuta huku staili zao zikiwa gumzo kama ile ya kubinua sehemu za nyuma na kunyanyua kijora na mguu mmoja. Shamila alijitahidi kujitetea kuwa umbea huo hajausambaza yeye, lakini hakuna aliyemuelewa, waliendelea kumsuta kwa staili ya kunyanyua mguu mmoja juu.

Gazeti la Ijumaa Wikienda lilipata nafasi ya kuzungumza na Khadija na kumuuliza kulikoni kumsuta shoga’ke namna hiyo ambapo alieleza kilichomkera; “Hakuna mwingine yeyote aliyesambaza umbeya huu bali ni huyuhuyu Shamila, ananiambia eti mimi nimeishiwa mpaka naishi na mume mwenye busha halafu ananiambia eti mimi nina mambo ya ki-Ambaruti.

“Yeye maisha yangu ya ndani yanamuhusu nini? Mbona yeye anatoka na kiongozi wa kundi la jogging na miye simtangazii? Maisha yangu na mume wangu ayaache na kama ni ushosti bora ufe siyo mambo ya kusambaziana umbea kwa mambo ya uongo, sipendi kabisa.”

Kwa upande wa msutwaji, Shamila alipotakiwa kueleza kwa nini alimtangazia shoga’ke mambo yake ya ndani alikanusha vikali na kusema hausiki na umbea huo na kusema Khadija alikuwa amemchoka tu ndiyo maana aliamua kumfedhehesha.

“Huo umbea anaousema Khadija wala sihusiki nao sema tu aliamua kuja kunifedhehesha kwa chuki zake na siyo kingine,” alisema Shamila.

Stori: Neema Adrian na Richard Bukos, Ijumaa Wikienda

Toa comment