The House of Favourite Newspapers

Aanzisha Bongo Dar es Salaam, Dude ataka kumgeuka!

0

dude2.gifMPENZI msomaji wa simulizi hii tamu ya Mrisho Mpoto, wiki iliyopita tuliishia pale Mrisho alipopata wazo la kutengeneza kipindi cha utapeli kwenye TV ambapo alifanikiwa kurekodi na kukubaliwa kukirusha katika Televisheni ya Taifa (TBC), baada ya hapo akaanza rasmi kutafuta nani awe mhusika mkuu.

Songa nayo sasa…

“Nikaenda moja kwa moja kwenye kikundi cha kuigiza kiitwacho, Splendid kipo Ilala, nikakutana na wasanii wengi lakini lengo langu lilikuwa ni ‘kumtageti’ msanii Kulwa Kikumba ‘Dude’ ambaye niliamini anaweza kuimudu sehemu hizo ambapo kipindi hicho alikuwa msanii wa kawaida tu ndani ya kundi hilo.

“Nikamwelezea idea yangu. Nikamwambia wewe muigizaji na mimi muigizaji, nakuomba tufanye kipindi kwenye TV na kila kitu nimeshafuatilia na kufanikiwa kupata TBC, lakini kikubwa ninachoomba tufanye biashara, mimi niwe dairekta na wewe muigizaji. Dude kusikia hivyo akakataa!”

Ehhh! Ananishtua kidogo. Dude atakataaje dili kama hili na yeye alikuwa msanii wa kawaida tu? Anagundua kaniacha njia panda, ananifafanulia zaidi.

“Dude alikuwa mbishi kwa sababu kule tayari kuna kipindi chao kilikuwa kikiruka akaniambia ‘ahha bwana unajua huku mimi ninapata airtime ya kutosha’. Nikamwambia hata huko utakapoenda airtime utapata tena ya kutosha. Basi akaniambia ukifanikisha nifuate nije kushiriki.

“Nikapata airtime nakumtafuta Dude ambapo tukaanza rasmi Kipindi cha Bongo Dar es Salaam. Kipindi kikawa maarufu sana. Kwa kuwa wote hatukuwa na gari, tukakutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Timu ya Yanga, Mohamed Binda tukaongea naye akatuuzia gari (Toyota Balloon).”

Gari moja? Mkawa mnaendeshaje sasa kaka maana mko wawili au mlikubaliana alimiliki mmoja?

“Ahhh haaa, ulikuwa kama mchezo, tulikuwa tukitengeana siku maalum ya kuliendesha. Wiki moja anaendesha Dude, wiki nyingine mimi, hivyohivyo na kama kutatokea dharura basi inabidi siku hiyo alichukue tu mwenye dharura.

“Sasa kwa kuwa Kipindi cha Bongo Dar es Salaam mmiliki nilikuwa mimi, nilikusanya fungu la kutosha na kununua gari jingine (Toyota Hiace), pia kuna mbunge alitokea anaitwa Faraja akasema anataka kununua vipindi vyote vya Bongo Dar es Salaam, nikamkusanyia vipindi vyote vya nyuma vilivyokuwa vimesharushwa na kumuuzia ambapo kama unakumbuka kulikuwa na CD kabisa za Bongo Dar es Salaam ambazo zilisambaa kwa wingi sana nchini.

“Ile pesa niliyopata kwa kuuza vipindi vya nyuma, nilinunua gari tena (Toyota Hiace) hivyo zikawa mbili nikamwachia Dude ile Hiace ya kwanza kwa hiyo kila mmoja akawa na gari yake lakini mimi nilikuwa na Hiace pamoja na Balloon.”

Safi sana Mpoto, safari ya Bongo Dar es Salaam ikaendeleaje baada ya kuanza kuwapatia mafanikio?

“Baada ya mafanikio mengi, tukaanza kupishana Kiswahili kidogo na Dude. Dude akawa anaongea mambo tofauti na wasanii wenzake, mara siku ambayo wanaandaa kipindi hataki niwepo wala kushiriki.”

Kwani Mrisho wewe sijawahi kukuona ukiigiza Bongo Dar es Salaam, sasa walikuwa hawataki uwepo kivipi?

“Sijawahi kuigiza lakini nilikuwa mshiriki tu, nilishawahi kumwambia Dude mimi muigizaji na wewe muigizaji tutagombania uigizaji mkuu na kama utakumbuka ushiriki wangu kwenye kipindi hicho nilihitaji nionekane mwishoni tu, na ukifuatilia kwa makini kila Bongo Dar es Salaam ilipokuwa ikiisha nilikuwa naonekana mwishoni kabisa nikiwa ndani ya mtumbwi.

“Basi kaka baada hapo, Dude akalewa sifa, akataka kunigeuka, akaenda TBC na kuanza kulalamika ‘Ohh nataka kujitoa, sitaki kufanya kazi na Mpoto nataka kufanya peke yangu, nipeni mkataba mpya.’ TBC wakamkatalia na kumwambia ‘Mwenye mkataba ni Mpoto hivyo hatuwezi kukatisha.’

JE, unajua  kitu gani kiliendelea kati ya Mrisho na Dude? Tukutane tena wiki ijayo hapahapa.

Leave A Reply