The House of Favourite Newspapers

Abdulrahman Babu: Alifanikisha Ujenzi Wa Tazara

0

Babu

Mwalimu Julius Nyerere akisalimiana na Profesa Abdulrahman Mohammed Babu (kulia) katika harakati zao za kuijenga nchi.

Reli ya TAZARA imechangia sana kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya China na Tanzania pia imekuwa njia muhimu za usafirishaji wa abiria na shehena za mizigo.

Tazara ni ufupisho wa Reli ya Tanzania na Zambia, neno hilo limekuwa ni alama ya urafiki wa dhati kati ya nchi tatu China, Tanzania na Zambia uliojengwa kwa damu na maisha na aliyefanikiwa ujenzi wake ni Profesa Abdulrahman Mohammed Babu.
Kwa sababu hii, Profesa Babu katika kitabu chake kingine, “An Economic Strategy for the Second Liberation of Africa”, anatoa wito kwa umma wa nchi za Kiafrika na za dunia ya tatu kwa ujumla, kuanzisha awamu ya pili ya mapambano ya ukombozi dhidi ya watawala vibaraka wa ukoloni mamboleo na moja ya njia ya kujikwamua ni ujenzi wa reli ya Tazara.

Babu rowing
Reli ya Tazara ulikuwa ni mradi mkubwa kabisa uliojengwa kwa msaada wa serikali ya China katika nchi za nje. Inaanzia Dar es Salaam, mji maarufu wa Tanzania na kuishia Kapri Mposhi, mkoa wa katikati wa Zambia, urefu wake ni kilomita 1,860. Kazi zote za ukaguzi na usanifu wa reli hiyo zilifanywa na wahandisi na wataalam wa China.

Mei 15, 1968, upimaji wa reli hiyo ulianza kufanywa nchini Tanzania baada ya Babu kurejea kutoka China alikotumwa na Mwalimu Julius Nyerere. Miaka kumi nyuma, Babu aliwahi kwenda China na alikuwa Mwafrika wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kukutana na viongozi wa China.
Mwaka huo 1968 Babu alitumwa na Mwalimu Nyerere nchini China kuzungumzia kuhusu reli hiyo ya Tazara. Akiwa China alikutana na viongozi wa huko akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Zhou Enlai (Cho En Lai) na akatoa wazo hilo, likafanikiwa.

Oktoba 26, 1970, ujenzi wa reli hiyo ulianza nchini Tanzania na Mwalimu akaenda China mwaka 1974 kumshukuru kiongozi wa China, Mao Tse Tung. Oktoba 22, 1975, reli ya Tazara ilikamilika na ilizinduliwa kwa majaribio ambapo Julai 23, 1976, ilianza kufanya kazi.

Ni nani huyu Babu?
Abdulrahman Mohamed Babu alizaliwa mwaka 1924 Zanzibar kwa baba mwenye asili mchanganyiko wa Mswahili na Mkomoro na mama wa familia mchanganyiko ya Kiarabu na Ki-Oromo kutoka Ethiopia. Wazazi wake walifariki akiwa na miaka miwili na kulelewa na shangazi yake eneo la Mji Mkongwe, Unguja.

Baada ya elimu ya sekondari, aliajiriwa kwenye Ushirika wa Zao la Karafuu kama karani, ambapo kwa kipato cha ujira duni, aliweza kujiwekea fedha za kujigharamia masomo nchini Uingereza mpaka akafikia ngazi ya uprofesa.
Mwanzoni alitaka kusomea uhasibu lakini akabadili nia akasoma falsafa na fasihi ya Kiingereza. Akiwa bado huko Uingereza, alijihusisha sana na siasa za kiharakati dhidi ya ukoloni na akachaguliwa kuwa katibu wa kamati ya harakati za Uhuru dhidi ya ukoloni kwa nchi za Afrika Mashariki na ya Kati (East and Central Africa Committee for Colonial Freedom).

Akiwa huko, yeye na wanaharakati wengine, Samir Amin, aliyekuja kuwa mhariri wa kwanza wa “The Tanganyika Standard” (sasa The Daily News) na Spika wa kwanza wa Bunge la Afrika Kusini huru, walihariri kwa pamoja jarida la Kiharakati la “Africa, Latin America, Asia Revolution” kudhihirisha hasira yao dhidi ya ukoloni mkongwe.
Karibu na mwisho wa miaka yake sita ya kuishi London, Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoanzishwa mwaka 1955, kilifanya mpango akapatiwa mafunzo juu ya organizesheni ya chama (party organization) na chama cha Leba cha Uingereza ili kumwandaa kwa harakati za uhuru visiwani; na aliporejea mwaka 1957, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ZNP, wakati huo Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) ndipo kilipoundwa kwa kuunganisha Chama cha African Association (AA) na Shirazi Association (SA), Februari 1957 na kujulikana, kwanza kama Afro-Shirazi Union (ASU) kabla ya kubadili jina kuwa Afro-Shirazi Party (ASP).
Katika Mapinduzi ya Zanzibar Babu hasa vijana wake wa Umma Party walishiriki na baada ya kufanikiwa kupindua alionekana akiwatafsiria maswali Rais Abeid Karume na John Okello katika mahojiano na mwandishi wa Uingereza. Aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Zanzibar na baadaye Waziri wa Mipango katika serikali ya Tanzania.
Babu alifariki katika Hospitali ya Chest, London Uingereza mwaka 1996, akazikwa Zanzibar

Leave A Reply