The House of Favourite Newspapers

Acha kulia! Kufilisika na kukwama siyo mwisho wa maisha!

0
Couple ignoring each other --- Image by © Lou Cypher/Corbis
Couple ignoring each other — Image by © Lou Cypher/Corbis

Leo nimeamua kuzungumza na wale ambao kwa namna moja au nyingine wamejikuta wakianguka na kupoteza kila kitu ambacho waliwahi kujikusanyia. Yaani wamefilisika na kubaki watupu na historia ya maisha yao imebadilika kabisa.

Pia nataka kuzungumza na wale ambao walikuwa na ndoto zao lakini wameshindwa kuzikamilisha kwa wakati baada ya kupoteza vitu muhimu kama kazi au kufiwa na watu ambao waliwategemea kuwa fikisha kwenye vilele vyao vya mafanikio.

Sasa wamekata tamaa na kuona kama hakuna njia au namna nyingine ya kuweza kunyanyuka na kupambana tena na maisha. Wanajichukia, wanaona maisha hayana thamani tena kwao, hiyo si sawa hata kidogo.

Mpenzi msomaji, hebu elekeza akili na mawazo yako yote hapa. Naamini leo hutaondoka kama ulivyokuwa kabla ya kuchukua gazeti hili. Tiba ya matatizo ya namna gani unaweza kuanza upya na kufikia tena kilele cha mafanikio, inapatikana leo hapa.

Katika maisha, kuna wakati utafikia hatua mbalimbali kubwa za mafanikio. Lakini pia, unaweza ukajikuta umepoteza vitu hivyo vyote na kurudi kama zamani au zaidi. Hayo ndiyo maisha.

Hata kama umepoteza kila kitu, kama umebaki na afya yako ikiwa imara, shukuru sana kwani huo ndiyo mtaji na ushindi mkubwa uliobakiza. Inawezekana kuanza upya. Kufilisika siyo mwisho wa maisha. Kupoteza ulichokuwa nacho siyo mwisho wa kila kitu.

Tayari imeshatokea, huwezi kubadili kitu. Sawa, umefilisika na hakuna jinsi. Sasa unadhani huo ndiyo mwisho wa maisha yako? Hapana! Maisha lazima yaendelee. Uhai lazima usonge, cha muhimu hapo ni kukubaliana na matokeo huku ukikaa chini na kutuliza akili.

Kama kuna mahali umejikwaa na kuanguka, nyanyuka haraka, jipanguse hilo vumbi na uendelee na safari. Kamwe usiendelee kupaangalia mahali ulipojikwaa. Hapakuhusu, achana napo. Songa mbele na mapambano ya maisha. Kuwa tayari kuanza upya.

Ikifika mahali huoni njia, basi itengeneze mwenyewe. Acha kulia. Kufilisika na kukwama katika mambo yako wala siyo mwisho wa maisha. Kaka, mama, baba, dada yangu naongea na wewe. Leo ni siku ya kukombolewa kwenye kifungo cha kukata tamaa.

Usiifikirie historia yako ya nyuma. Mafanikio yako hayako nyuma, bali mbele unakoelekea.

Achana na historia mbaya ya huko nyuma. Hicho ulichokipoteza, unaweza kurejesha zaidi ya hicho! Hayo ndiyo maisha. Kama njia ya kwanza imeshindwa kukufikisha unapotaka kwenda ni wajibu wako sasa kutengeneza njia nyingine.

Mtu mmoja anaitwa W. Mitchell. Huyu ni mwandishi wa vitabu. Yeye aliwahi kupata ajali mbaya sana ya ndege. Akapoteza miguu yote na kupooza kuanzia shingoni hadi kiunoni! Akafilisika mali zote baada ya kuingia madeni makubwa wakati wa kutibu majeraha na afya kwa ujumla.

Lakini Mitchell alianza upya kwa kuwatia watu moyo. Akawa anazungumza akiwa kwenye kiti cha kusukuma cha matairi.

Akihamasisha watu kujikomboa na umaskini. Leo hii ni bilionea mkubwa duniani

Hayo ndiyo maisha. Maisha yamekupiga mwereka? Unaweza kusimama tena. Yaani siyo kusimama tu, unaweza kujikusanyia mali zaidi ya ulizokuwa nazo huko nyuma.

Wakati mwingine Mungu humfilisi mtu kwa makusudi pengine ili ajifunze kuishi maisha ya chini. Nyanyuka, pambana kuanzia hapo na naamini utaandika tena historia ya kati ya watu walioanguka lakini wakasimama tena!

Leave A Reply