The House of Favourite Newspapers

Acha kutamani vya nje, mtengeneze wako awe bora!

NI Ijumaa nyingine tuliyoj-aaliwa na Mwenyezi Mungu. Karibu kwenye uwanja wetu huu wa kupeana elimu juu ya uhusiano na maisha kwa jumla.  Katika suala la uhusiano wa kimapenzi, baadhi ya wanaume wanasukumwa zaidi na tamaa za miili yao wakati wanawake wanasukumwa na hisia za ndani za upendo. Pengine hii ndiyo sababu inayofanya wanaume wengi washindwe kujizuia wanapotembea barabarani na kukutana na mwanamke mrembo au mwenye shepu yake matata.

Hata kama hawatapata nafasi ya kuzungumza nao chochote, lakini wengi hushindwa kujizuia na kugeuza shingo zao nyuma! Kinachowafanya baadhi ya wanaume wageuza shingo zao hata kama wapo na wake au wapenzi wao, ni zile tamaa za kibinadamu walizoumbwa nazo; kupenda vitu vizuri.

Ukifuatilia kwa karibu na umakini, utagundua wanaume wengi wana udhaifu mkubwa mno kwa wanawake wanaojipenda, wanaovaa na kupendeza, wanaonukia vizuri na wanaojiweka ‘smart’. Pengine ndiyo sababu ‘nyumba ndogo’ nyingi zinakuwa na sifa hizi nilizozitaja na kuwateka vilivyo waume wa watu.

Mtu ana mke au mchumba wake, anashindwa kumtengeneza kimuonekano awe vile ambayo yeye anataka kwa sababu kama ukimpenda mwanamke, utamtengeneza kuwa vile unataka. Matokeo yake anakuwa ni mtu wa kutamani wanawake hovyo barabarani! Haoni kama anayo nafasi ya kumtengeneza mke wake au mchumba wake, akawa kama hao anaowatamani huku barabarani, kanisani, sokoni, kazini na wengine hufikia hata hatua ya kutamani wanawake wanaohudumia kwenye baa!

Hiyo ipo pia kwa baadhi ya wanawake! Lakini kwa kuwa wao wanaongozwa zaidi na hisia, ni nadra kumuona mwanamke akigeuza shingo yake barabarani kumtazama mwanaume hata kama ana mvuto, ana mwili wa mazoezi au amependeza kiasi gani.

Wameumbwa na uso wa haya au aibu, lakini hiyo pia haiwazuii kutamani ndani ya mioyo yao kwamba ‘mume wangu angekuwa kama huyu ningeringa!’ Wanaishia kuumia ndani ya mioyo yao, hawajui kwamba wanayo nafasi ya kuwabadilisha waume zao au wachumba zao wakawa na mwonekano ambao wanautamani kwa wanaume wengine.

Wanachoshindwa kutambua wengi ni kwamba unapokuwa na mume kama wewe ni mwanamke, jukumu la kumfanya apendeze na kuvutia, awe kama unavyotaka awe, ni la kwako. Na kama wewe ni mwanaume, jukumu la kumfanya mkeo au mchumba wako apendeze na kuvutia kama unaowatamani, ni la kwako.

Hii haihitaji uwe na mamilioni ya fedha kubadili mwonekano wa mwenzi wako, ni suala la upendo na kujitoa kwako tu kama kweli unampenda na una malengo naye. Kama wewe ni mwanamke, hebu jiulize; ni lini ulimnunulia mumeo shati zuri, suruali au hata viatu (hata kama ni vya mtumba) ambavyo vitamfanya na yeye aonekane mwanaume wa kupendeza mbele ya wanaume wenzake? Kama wewe ni mwanaume, je, unamgharamia mkeo inavyostahili ili aonekane mrembo? Lini ulimpa fedha za kwenda saluni kutengeneza nywele zake vizuri? Lini ulimnunulia pafyumu au mafuta mazuri au nguo nzuri za kumfanya apendeze mbele ya wengine?

Bila shaka majibu utakuwa nayo mwenyewe. Usimfanye mwenzi wako ‘akafubaa’ kwa kukosa matunzo wakati wewe uko bize kutamani wengine wa barabarani. Mtengeneze mwenzi wako awe vile unavyotaka, kwanza utajisikia kuwajibika kikamilifu, utajikuta ukizidi kumpenda na kubwa zaidi, utamfanya na yeye akupende zaidi kwa sababu ataona unamjali. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.

Comments are closed.